Jumatatu, 16 Desemba 2024

WATUMISHI MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA BIASHARA WATEMBELEA KITUO CHA WATOTO YATIMA KIGAMBONI

Na AMINA SAIDI-Mahakama ya Biashara

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, chini ya uongozi wa Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Cleophace Morris, hivi karibuni walitembelea Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Hisani Orphanage Centre kilichopo wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni sehemu ya matendo ya huruma yaliyosheheni msaada kwa watoto yatima katika kipindi kuelekea mwaka mpya. Watumishi hao walikabidhi fedha na mahitaji muhimu ili kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokikumba kituo hicho katika utunzaji wa watoto 84 wanaolelewa hapo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Morris alionesha furaha kubwa alipoona watoto hao wakipokea misaada hiyo kwa shukrani na furaha, na pia alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwatembelea watoto na kuwaunga mkono.

"Tunapaswa kuendelea kuwa na moyo wa huruma na kutoa msaada kwa watoto hawa ili tuwasaidie kufikia malengo yao na kuwa na maisha bora zaidi," alisema, huku akihimiza mshikamano wa kijamii na uhisani kwa watoto yatima na watu walioko katika mazingira magumu.

Mlenzi wa Kituo hicho, Bi. Hidaya Mtalemwa, alitoa shukrani za dhati kwa Mahakama Kuu na wahisani wote walioshiriki katika ziara hiyo.

Bi. Mtalemwa alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwatunza watoto na kuwapa fursa ya kufikia malengo yao ya baadaye. Aliwahimiza watu waendelee kujitolea ili watoto hao waweze kuishi katika mazingira bora na salama.

Hii ni sehemu ya juhudi za kila mwaka zinazofanywa na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara katika kuunga mkono jamii na kusaidia watoto yatima kwa kutoa michango ya fedha, vifaa vya shule, mavazi, na mahitaji mengine muhimu.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Cleophace Morris (kushoto) akimkabidhi Bi. Hidaya Mtalemwa (katika picha ya juu na chini) baadhi ya misaada iliyowasilishwa kituoni hapo.


Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara wakiwa ndani ya usafiri kuelekea katika kituo cha Hisani Orphanage Centre.

Sehemu ya watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Hisani Orphanage Centre.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama, walezi wa kituo pamoja na watoto yatima, katika zoezi ya kukabidhi misaada iliyowasilishwa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni