Jumatatu, 16 Desemba 2024

JAJI MFAWIDHI IRINGA AWAPONGEZA MAHAKIMU KWA KUJIENDELEZA KIELIMU

Na. LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama, Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru amewapongeza Mahakimu watatu ambao wametunukiwa Shahada za Uzamili katika fani ya Sheria na Chuo Kikuu cha Iringa kwa hatua hiyo ya kujiendeleza kielimu.

Mhe. Ndunguru alitoa pongezi hizo hivi karibuni katika hafla fupi ya chakula cha jioni alichokiandaa kwa ajili ya Mahakimu hao, Mhe. Venus Cronery Rwetambura, Mhe. Angela Kanyanyinyi na Mhe. Ayubu Shellimo katika Hotel ya Sunset iliyopo maeneo ya Gangilonga ndani ya Manispaa ya Iringa.

Mhe. Rwetembura ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na kwa sasa ni Msaidizi wa Sheria wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Byera ni Hakimu Mkazi na kwa sasa anafanya kazi katika Mahakama ya Mwanzo ya Mwanjelwa iliyopo jijini Mbeya na Mhe. Shellimo ni Hakimu Mkazi ambaye kwa sasa anafanya kazi Mahakama ya Mwanzo ya Uyole iliyopo jijini Mbeya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ndunguru alisema, “Nimeona ni busara nikawaita hapa ili tukae hapa pamoja katika hii tafrija ndogo ili kwapongeza kwa kujiendeleza kielimu. Kwa kweli nimefurahi sana maana mimi ni muumini wa watu wapenda elimu. Nategemea elimu yenu mliyojiongezea inakwenda kuwa na tija kwenu, kwa mahakama na nchi pia.”

Jaji Mfawidhi alitumia fursa hiyo kuwahimiza Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama kuwa na moyo wa kujiongezea elimu. “Tusiwe watu wa kuridhika na elimu ndogo, badala yake tujikuze kielimu ili kujiongezea maarifa kwenda sambamba na mabadiliko ya kidunia,” alisema.

Akiongea kwa niaba ya Mahakimu wenzake, Mhe. Rwetembula alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa tafrija hiyo ya pongezi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru akisisitiza jambo wakati akiongea na Mahakimu (waliokuwa pamoja na familia zao) wakati wa chakula cha usiku alichowaandalia ili kuwapongeza kwa kujiendeleza kielimu.

Msaidizi wa Sheria wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Verus Cronery Rwetembula akitoa neno wakati wa hafla hiyo.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa iliyopo jijini Mbeya, Mhe. Angela Kanyanyinyi Byera akitoa neno wakati wa hafla hiyo ya chakula cha usiku.

Mhe. Ayubu Shellimo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Beda Ndunguru (wa pili kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu walitunukiwa Shahada za Uzamiri katika fani ya Sheria. Kutoka kushoto ni Mhe. Verus Rwetembula, Mhe. Ayubu Shellimo na Mhe. Angela Kanyanyinyi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni