Jumapili, 15 Desemba 2024

MMEBEBA MAISHA YA WATU, KATENDENI HAKI; MSAJILI MKUU

Na Yusufu Ahmadi – IJA, Lushoto

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya amewaasa Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo nchini kwenda kutenda haki katika kazi yao ya utoaji haki kwa kuwa kazi hiyo imebeba hatma ya maisha ya watu.

Mhe. Eva ametoa wito huo tarehe 13/12/2024 wakati kufunga mafunzo elekezi yaliyokuwa yanatolewa kwa Mahakimu hao 88 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambayo yalifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 02/12/2024.

Amewaasa kwenda kuandika hukumu ambazo zitatatua migogoro, kujibu hoja zinazoletwa Mahakamani, na sio kwenda kuzalisha migogoro huku akisema: “Tukumbuke maamuzi yetu yameshika maisha na mali za watu.”

Pia amesema kuwa taifa lina matarajio makubwa na Mahakimu hao na hivyo kuwataka kwenda kutenda haki kwa wakati na bila ubaguzi wowote.

“Taifa lina matarajio makubwa kwenu, hivyo mnatakiwa kutenda haki kwa wakati na bila ubaguzi wowote, kuheshimu na kutii Katiba na Sheria za nchi na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati,” amesema Msajili Mkuu.

Vilevile Mhe. Eva amewahimiza Mahakimu hao kuzingatia uadilifu na maadili katika kazi yao kwa kujiepusha na matendo yote yatakayoharibu haiba na uadilifu wao. 

Aidha, Msajili Mkuu amewasihi Mahakimu hao kusoma kwa bidii, akisema kuwa uweledi hauendi bila mtu kusoma huku akiwashauri kufuatilia mafunzo mbalimbali yanayoendeshwa na IJA  hususani ya mtandaoni. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amesema kuwa mafunzo hayo yameenda vema ambapo washiriki wamepitishwa kwenye mada muhimu zilizowaandaa vema katika utekelezaji wa kazi yao hiyo mpya.

Naye Hakimu Mkazi Mhe. James Mwakalosi akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, ameushukuru uongozi wa Chuo na Mahakama kwa ujumla kwa kuwapatia mafunzo hayo akibainisha kuwa yamewapa mbinu na maarifa muhumu yatakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao mapya.

Maafisa mbalimbali wa Mahakama wamehudhuria hafla hiyo ya ufungaji akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akimkabidhi cheti cha ushiriki mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akihutubia wakati wa ufungaji wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 88 wa Mahakama za Mwanzo nchini katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) tarehe 13/12/2024.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (katikati waliyokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Mahakimu wakazi wapya. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (katikati waliyokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Mahakimu wakazi wapya. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka akizungumza katika mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mhe. James Mwakalosi akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake katika mafunzo hayo.




Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akitoa neno la utangulizi wakati wa mafunzo hayo elekezi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni