- Watembelea vituo viwili vya Watoto wenye uhitaji.
- Watembelea Hifadhi
ya Taifa Mikumi.
Na
MWANAIDI MSEKWA-Mahakama ya Kazi
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph
Mlyambina hivi karibuni aliongozo viongozi na watumishi wa Divisheni hiyo
kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji katika Mkoa wa Morogoro kwenye kituo cha
Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kituo cha kulelea watoto walemavu wa akili
na afya ya mwili.
Safari ya kuelekea Morogoro ilianza majira ya afajiri tarehe 29 Novemba, 2024 kwa usafiri wa treni ya kisasa ya mwendo kasi, maarufu kama SGR, kwa viongozi na watumishi wote walipanda daraja la kawaida, ikiwa ni ishara ya umoja na upendo miongoni mwao. Ndani ya behewa, Mhe. Dkt. Mlyambina aliongoza mchezo wa karata ikiwa ni moja ya kufurahia safari ya pamoja.
Msafara
huo uliwasili katika Stesheni ya Jakaya Kikwete Morogoro majira ya saa 1:50 asubuhi
na kupokelewa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki Morogoro, wakiwemo Naibu Msajili, Mhe. Suzan Philip Kihawa, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mhe. Asha Hassan Waziri na Mtendaji, Bw.
Ahmed Suleiman Ng’eni.
Baada ya mapokezi na kupata kifungua kinywa katika hoteli ya Hot land iliyopo maeneo ya Nane Nane Morogoro, Jaji Mfawidhi aliongozo ujumbe wake kuelekea kituo cha kwanza cha Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege kilichopo Kata ya Saba Saba Morogoro Mjini na kupokelewa na Mwalimu Mkuu wa Shule, Bib. Dotto Kangeta.
Majaji
wakiongozwa na Jaji Mfawidhi walisaini kitabu cha wageni ambao ni Mhe. Dkt.
Modesta Opiyo na Mhe. Biswalo Mganga. Walikuwepo pia Naibu Wasajili wa Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi; Mhe. Enock Matembele, Mhe. Mary Mrio na Mhe. Rita Tarimo
na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Jumanne Muna.
Wakiwa katika Kituo hicho, watumishi hao wa Mahakama walipata taarifa fupi kutroka kwa Bi. Kangeta aliyelezea historia fupi ya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege. Alisema shule ina watoto 1,111, kati ya hao wapo watoto wa kawaida na watoto wenye matatizo ya afya 123, watoto wenye matatizo ya kusikia, watoto wenye usonji na watoto wenye ulemavu wa akili.
Aliendelea kwa kusema shule ina walimu 33 mchanganyiko, wanaume kwa wanawake na walimu wengine wapo masomoni. Baadaye, Jaji Mfawidhi alielezea dhumuni la safari yao kuja kuwaona watoto wote wanaopata elimu na huduma mbalimbali katika shule hiyo.
Aliendelea kwa kusema kuwa wakiwa sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa pamoja wanaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Serikali katika kuwezesha upatikanaji wa elimu na huduma mbalimbali kwa watoto hao.
“Nasi tukiwa sehemu ya jamii ya Watanzania kwa umoja wetu tunatoa zawadi mbalimbali na fedha taslimu kwa ajili ya maendeleo ya watoto na shule,” alisema huku akinukuu Maandiko Matakatifu kutoka 2 Wakorintho 1:4 yanayosema, “Atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi kupata kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunafarijiwa na Mungu”.
Viongozi na watumishi walipata fursa ya kuwaona watoto wenye matatizo ya kusikia. Watoto hao waliwakaribisha kwa kuimba nyimbo ya Taifa, tukio ambalo liliwafurahisha viongozi na watumishi wote waliohudhuria safari hiyo na kuguswa na huduma inayotolewa kwa watoto hao na kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayofanya.
Baada ya kutembelea kituo hicho, Mhe. Dkt. Mlyambina aliongoza msafara wake kuelekea kituo cha kulea watoto wenye ulemavu kilichopo Mvomelo. Safari hiyo iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor, ambaye aliambatana na Jaji wa Mahakama ya Tanzania Morogoro, Mhe. Steven Magoiga.
Majaji, Naibu Wasajili, Mtendaji na watumishi waliwasili majira ya mchana kituoni hapo na kupokelewa na watoto na walezi wao kwa nyimbo nzuri, zilizofuta uchovu wa safari ya masaa mawili kwa wageni hao. Watumishi waliungana na watoto kwa kuimba na kucheza kitu kilichovutia watu wote waliohudhuria safari hiyo.
Wakiwa katika kituo hicho, wageni hao walipata taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Kituo, Bi. Bakita ambaye pia ni mwanzilishi, alielezea kuwa wanahudumia kaya 600 katika Wilaya za Morogoro. Aliendelea kusema kuwa kwa sasa kituo kinafadhiliwa na Chama cha Mawakili na Wadau mbalimbali waliopo katika Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza akiwa katika Kituo hicho, Mhe. Dkt. Mlyambina alisema wao ni sehemu ya jamii na wameguswa na huduma zinazotolewa na kituo hicho na kuwasilisha zawadi ambazo zimetokana na michango ya watumishi kwa kujitoa ili kushiriki katika utoaji huduma kwa jamii. Zawadi hizo ni vyakula na fedha taslimu kwa ajili ya matibabu.
Baada ya matukio hayo mafupi kukamilika, viongozi na watumishi walianza safari ya kurejea Morogoro Mjini kwa ajili ya shughuli nyingine iliyoandaliwa, ikiwemo bonanza la kirafiki kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi na Mahakama ya Tanzania Kanda ya Morogoro.
Bonanza hilo lilifanyika katika Kiwanja cha Jamuhuri kuanzia saa 11 jioni na michezo mbalimbali ilichezwa, ikishirikisha viongozi na watumishi. Katika mchezo wa mpira wa miguu,Timu ya Mahakama Morogoro iliwanyanyasa wapinzani wake kwa mabao 4 - 0.
Katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume, Timu ya Mahakama ya Kazi ilishinda kwa kuwavuta wenyeji wao, huku Kamba wanawake Mahakama ya Morogoro ikaibuka kidedea. Vile vile katika mchezo wa kufukuza kuku wanaume, Timu ya Mahakama ya Kazi iliibuka na ushindi na timu ya wanawake Mahakama ya Morogoro nayo iliondoka na kuku.
Upande wa mpira wa pete, Timu ya Mahakama Morogoro ilitupia vikapu 13 – 3. Bonanza hilo lilifana na kukidhi matarajio yaliyokusudiwa, ikiwemo watumishi kufahamiana na kushiriki mazoezi kwa pamoja ili kuimarisha afya ya akili na mwili kwa maendelo ya Taifa na Mahakama ya Tanzania.
Siku ya pili, Viongozi na watumishi wa Mahakama ya Kazi mapema asubuhi walianza safari ya kuelekea Hifadhi ya Taifa Mikumi na wakafanikiwa kuwaona Wanyama mbalimbali, wakiwemo Tembo, Twiga, Pwala, pundamilia, Nguruwe pori (kasongo yeye), Simba, Viboko, Mamba, Kifaru na aina mbalimbali za ndege wa mwituni.
Baada ya safari Mikumi kukamilika, viongozi na watumishi walirejea Morogoro mjini kwa ajili ya mapumziko na jioni kuhudhuria tafrija fupi iliyoandaliwa na Kamati ya Huduma ya Jamii chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Mganga. Tafrija hiyo ilifanyika katika Hotel ya Hot land iliyopo Nane Nane Morogoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina akiongoza
mchezo wa karata ndani ya behewa la treni ya mwendo kasi katika safari ya
kuelekea mkoani Morogoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, wakisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Bi. Dotto Kangeta mara baada ya kuwasili shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Bi. Dotto Kangeta akiwakaribisha wageni wake shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Bi. Dotto Kangeta akieleza shukrani zake kwa wageni baada ya kupokea zawadi mbalimbali.
Msafara kuelekea Mvomelo
katika Kituo cha kumbukumbu ya Erick kwa ajili ya kutoa elimu na marekebisho
kwa walemavu.
Mwanzilishi wa Kituo cha EMFERD Bibi Bakita (hayupo kwenye picha) akiwakaribisha wageni katika kituo hicho.
Majaji wakiwasilisha zawadi za watoto kwa Mwanzilishi wa Kituo cha EMFERD Bibi Bakita.
Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi (juu na picha mbili chini) wakiwa katika matembezi ya Royal Tour kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi Morogoro.
Michezo mbalimbali ikiendelea katika uwanja wa Jamuhuri Morogoro (juu na pixcha mbili chini).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni