TANZIA
Mahakama
ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake Mhe. Maximillian Alphonce
Malewo aliyekuwa Naibu Msajili akihudumu katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam. Marehemu Mhe. Malewo alikuwa pia ni Hakimu
Mwenye Mamlaka ya Nyongeza ya Kusikiliza Mashauri ya Mahakama Kuu.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
marehemu Mhe. Malewo alikutwa na umauti mnamo tarehe 17 Desemba, 2024 majira ya
saa moja usiku wakati alipokuwa amelazwa akipatiwa huduma ya matibabu katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo Mloganzila mkoani Dar es Salaam baada ya
kuugua na kulazwa. Marehemu anatarajiwa kuagwa tarehe 20 Disemba, 2024 Misugusugu
Kibaha Mkoani Pwani na atazikwa tarehe 21 Disemba, 2024 Himo Kilanja- Kilimanjaro.
Aidha, marehemu Mhe. Maximillian Alphonce Malewo
alizaliwa mnamo tarehe 28 Julai, 1975. Aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania
tarehe 03 Januari, 2002 kama Hakimu Mkazi Daraja la III na kupangiwa Kituo cha
Kazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma alihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka
2006. Mnamo mwaka 2006 hadi 2009 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama
ya Wilaya Mbinga. Mwaka 2009 aliteuliwa kuwa Naibu Msajili na kupangiwa Mahakama ya Rufani alipohudumu hadi 2015.
Vilevile,
Akiwa anaendelea na wadhifa wake wa Naibu Msajili, mwaka 2015 hadi 2016
alipangiwa kuhudumu Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Mwaka 2016 hadi 2021
alipangiwa kuhudumu Mahakama Kuu Kanda ya Songea. Mwaka 2021 alipangiwa
kuhudumu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na mnamo Julai, 2024 alipangiwa kuhudumu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mpaka mauti yalipomfika.
Mahakama
ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki kuomboleza msiba huu wa
kuondokewa na mpendwa wetu.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA
LIHIMIDIWE.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni