Jumatano, 18 Desemba 2024

'KUTELEKEZA MTOTO NI KOSA LA JINAI'

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Sameera Suleiman amesema ni kosa la jinai kwa mzazi kutelekeza mtoto wake bila kutoa matunzo huku akitaja adhabu yake kuwa ni faini au kifungo kisichopungua miaka mitano jela kwa mujibu wa kifungu cha 166 cha sheria ya  kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marekebisho kwa 2019.

Mhe. Sameera alieleza hayo jana tarehe 17 Desemba, 2024 wakati akitoa elimu ya Mahakama katika kipindi cha Gumzo Leo kinachorushwa na Radio Chalinze Fm iliyopo Wilaya Chalinze mkoani Pwani. 

Mhe Sameera alisema jukumu la kutunza mtoto ni la baba lakini malezi ni ya wazazi wote wawili.

Aliongeza kuwa, katika Mahakama ni mara chache kuona mwanaume anafika mahakamani kudai matunzo ya watoto kwa mama japo sheria inaruhusu endapo baba atakua mgonjwa au hajiwezi na mama ana uwezo na hahudumii.

Akizungumza katika kipindi hicho naye Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Vedastus Mwaria alisema sheria inamtambua baba ndio mzazi mwenye wajibu wa kutunza Watoto.

“Malezi ya watoto ni wazazi wote wawili lakini jukumu la kutunza watoto ni la baba,” alisema Mhe. Mwaria.

Mhe. Mwaria alisema tofauti za wazazi, watoto hawapaswi kuzijua na kuongeza kuwa ugomvi wa wazazi usihusishe watoto kwakuwa watoto wanapaswa wamtambue baba na mama mpaka watakapokua watu wazima watambue wenyewe.

Akijibu swali lililoulizwa na Mtangazaji wa kipindi hicho, Bi. Zaibnab Ngambila kuhusu baba kumuona mtoto ambaye hamhudumii, Mhe. Sameera alisema shauri linapofika mahakamani hata kama haijaisha baba ana haki ya kuwaona  watoto wake hata kama hawahudumii na kuionya jamii haswa wazazi wa kike kuepuka kuwapandikiza watoto ubaya kwa mzazi wa kiume kwa sababu hawahudumii.

Akijibu swali lingine kuhusu mikopo ya riba lililoulizwa na Mtangazaji, Mhe. Mwaria alitoa ufafanuzi kwamba kukopa sio kosa kama mkopeshaji yuko kisheria yaani ana leseni ya bishara ya kukopesha.

Mfawidhi huyo aliwaasa wananchi katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kutokukopa kwa ajili ya kununua nguo bali wakope kwa ajili ya kuzalisha ili iwe rahisi kurudisha mkopo pamoja na riba yake, vilevile  amewataka wakopaji kusoma vizuri masharti ya mkopo ili kuona kama uwezo wa kulipa kwa muda uliowekwa upo.

Lengo la kushiriki katika kipindi hicho ni pamoja na kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo kuzifahamu sheria mbalimbali ili kuepuka kuingia kwenye mkono wa sheria.

Mkazi Mwandamizi  Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe.  Sameera Suleiman Hakimu (kulia) na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya  Bagamoyo, Mhe. Vedastus Mwaria wakitoa mada katika kipindi cha Gumzo Leo cha Chalinze Fm iliyopo Wilaya ya Chalinze jana tarehe 17 Desemba, 2024.

Hakimu Mkazi Mwandamizi  wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe.Vedastus Mwaria akitoa mada katika Kituo cha Radio cha Chalinze  FM jana tarehe 17 Desemba, 2024.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo (wa pili kulia), Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Vedastus Mwaria, Mwakilishi wa Habari wa Mahakama Pwani, Bi. Eunice Lugiana (wa tatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Watangazaji wa Redio Chalinze Fm.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni