Na ARAPHA RUSHEKE –Mahakama, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewakumbusha
watendaji kusimamia maslahi ya watumishi wenye mahitaji maalum.
Mhe Kikwete ametoa rai
hiyo jana 17 Desemba, 2024 katika ukumbi wa OSHA Dodoma alipokuwa anafunga
mafunzo ya watumishi wenye mahitaji maalum kutoka Serikalini, Mahakama na
Taasisi za Umma.
Mafunzo hayo yaliendeshwa
na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kwa kushirikiana na Taasisi ya
OSHA inayosimamia Usalama na Afya Mahala pa Kazi.
“Nimefarijika kuona mafunzo haya yamejumuisha Mhimili
wa Mahakama ili kuwajengea uelewa washiriki katika masuala ya usalama na afya
waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia kanuni bora na
kujilinda dhidi ya viatarishi vya magonjwa na ajali mahala pa kazi,” amesema.
Mhe. Kikwete aliwaambia washiriki wa mafunzo
hayo kuwa yeye binafsi na Wizara wanaamini changamoto nyingi zinazojitokeza
mahala pa kazi zitatatuliwa kama wataitumia vizuri elimu waliyoyapata.
“Niwatake watendaji
kuhakikisha haki na maslahi ya watumishi wenye mahitaji maalum yanasimamiwa kwa
kutunga sera na mipango mbalimbali ikiwemo inayowezesha sera hizo
kutekelezeka,” alisema.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Joseph Mlyambina, akizungumza
wakati wakutoa neno fupi la shukrani, aliwakumbusha washiriki ujumbe wa Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakati
wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Alisema kuwa Jaji
Kiongozi alimsihi kila mtumishi wa umma kuongozwa na mambo matatu ambayo
Mahakama imeamua kuweka kwenye salamu yake ambayo ni uadilifu,weledi na
uwajibikaji.
Mada mbalimbali
ziliwasilishwa wakati wa mafunzo hayo ambayo yalitolewa kwa siku mbili kuanzia
tarehe 16 Desemba, 2024, ikiwemo utangulizi wa awali kuhusu OSHA Tanzania na
shughuli na majukumu yake na mfumo wa kisheria unaosimamia ajira na mahusiano kazini
kwa watu wenye mahitaji maalum
Nyingine ni mapitio ya kina ya sheria ya OSHA katika kulinda watu wenye mahitaji maalum; kuvifahamu vihatarishi na madhara yake kwa wafanyakazi wenye mahitaji maalum na changamoto za msongo wa mawazo na afya ya akili.
Meza kuu wakati wa
kufunga mafunzo hayo ikiongozwa na mgeni
rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete.(aliyekaa katikati). Kushoto kwake ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina,
anayefuatia ni Jaji Mahakama Kuu kutoka Divisheni
hiyo, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, kulia kwake ni Kamishna wa kazi Tanzania Bara,
Bi Suzan Mkangwa, anayefuatia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala
pa Kazi, Bi. Hadija Mwenda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza
wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Joseph Mlyambina, akiongea neno la
shukrani wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi, Bi. Hadija Mwenda (aliyesimama) akitoa neno la shukrani.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na na watumishi wa Mahakama waliohudhuria mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni