SALUM TAWANI na MAGRETH KINABO – Mahakama, Dar es Salaam
. Yajivunia ongezeko la Majaji na Mahakimu wanawake
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kimesema kinatarajia kufanya maadhimisho ya miaka 25 jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 23 Januari , 2025 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 19 Desemba, 2024 kuhusu maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chama hicho ambapo pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Barke Mbaraka Sehel Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Haki Utoaji Haki Jumuishi Kinondoni, (Integrated Justice Center).
Jaji Sehel amesema kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho hayo, utakaofanyika tarehe 20 Januari, 2025 anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Jijini Arusha katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).
Ambapo amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo, ni “Kusheherekea Utofauti na Mshikamano Katika Usawa wa Jinsia”.
‘’Maadhimisho haya yatakusanya wadau mbalimbali wakiwemo wanachama wa TAWJA, waliopo kazini na walio wastaafu, Majaji na Mahakimu wa Kike kutoka katika Mahakama za Tanzania na Zanzibar. Pia Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho.
Wengine ni washiriki wa Kimataifa kama vile UN Woman, UNDP, UNICEF na wadau wa maendeleo, wawakilishi kutoka Serikali ya Tanzania Bara na Visiwani wakiwemo viongozi wa Wizara ya Katiba Sheria, mashirika ya haki za wanawake kama vile TAWLA , WLAC, TGNP, NGOs na vikundi vya utetezi,mashirika mbalimbali kama vile Balozi , taasisi za kifedha na vyombo vya habari.
Jaji Sehel ameongoza kuwa TAWJA ilianzishwa mwaka 2000 baada ya majadiliano kati ya Marehemu Justice Patch na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania,Mhe. Eusebia Munuo, kama mshirika wa Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake (IAWJ) TAWJA inajikita katika kukuza haki za wanawake, kuhakikisha usawa wa kijinsia katika utawala wa Sheria na kutetea haki sawa kwa wote, hasa wanawake na watoto.
Amefafanua mafanikio ya miaka 25 yanayosheherekewa yaliyofikiwa katika maeneo hayo ni makubwa na TAWJA imetoa mchango mkubwa katika usawa wa kijinsia ndani ya mfumo wa Mahakama ya Tanzania na juhudi zake za kuboresha haki za wanawake na makundi dhaifu. Hivyo hadi sasa kwa mafanikio hayo ya TAWJA yanawafanya tuzingatie maendeleo yaliyofikiwa na kazi endelevu inahitajika ili kuendeleza mfumo wa kisheria wenye usawa unaojumuisha wote.
‘’Tunawakaribisha washiriki kuja Arusha ili kutafakari mafanikio ya miaka 25 ya TAWJA na kujadili changamoto za baadae katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kwa pamoja,’’ alisisitiza Mwenyekiti huyo Mhe. Jaji Sehel.
Aidha Jaji Sehel ametanabaisha kuwa katika maadhimisho hayo, kutakuwa na shughuli mbalimbali kama vile mbio za TAWJA, zitakazofanyika tarehe 19 Januari, 2024 na kauli mbiu yake ni ‘Mshikamo katika haki za kijinsia uaanzia hapa shiriki na elimisha. Mgeni rasmi katika mbio hizo anatarajia kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja Mabunge ya Duniani(IPU) Mhe.Dkt. Tulia Ackson.
Hivyo lengo la mbio hizo ni kushirikiana kwa pamoja katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kijinsia na kuongeza uelewa katika jamii kuhusu ukatili wa kijinsia (GBV), ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na haki za wanawake katika umiliki wa ardhi. Pia fedha zitakazokusanywa kwenye mbio hizo zitasaidia kuanzisha klabu za haki na jinsia katika shule za sekondari sita zilizopo jijini Arusha kwa ajili ya kutoa elimu ya kijinsia na uendelezaji wa ujuzi wa maisha.
Mhe. Jaji Sehel katika kesi zinazohusiana na masuala ya kijinsia katika miaka ya sasa zinazoongoza ni za ubakaji na kuingiliana kinyume na maumbile, ambapo zipo katika kila mkoa tofauti na zamani zinaripotiwa kwenye fulani.
Naye Mwenyekiti wa Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Jaji Mstaafu wa MahakamaKuu ya Tanzania, Mhe. Sophia Wambura aliyataja mafaniko yaliyotokana na juhudi za chama hicho kuwa kuongezeka kwa idadi ya majaji na mahakimu wanawake ukilinganisha na zamani.
Mhe. Jaji Wambura alitolea mfano kuwa kwa upande wa Mahakama ya Rufani Tanzania mwaka 2000 kulikuwa hakuna Jaji mwanamke, lakini sasa kuna majaji 36 kati ya hao wanawake wako 13, na upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuna majaji 110 kati yao majaji wanawake 41.
Amezitaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kama majaji na mahakimu kuwa kesi nyingi za namna huharibika kutokana baadhi ya familia kutoa ushirikiano kwa Mahakama kwa sababu ya mahusihano yaliyokuwepo kati ya mtendakosa na aliyetendewa, Pia kuairishwa kwa kesi mara kwa mara kunasababisha wahusika katika kesi za masuala kushindwa kufika mahakamani kwa sababu za ukosefu fedha na kutenga muda wa kazi na kifamilia.
Akizungumzia kuhusu matukio yatakayofanyika katika maadhimisho hayo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Aisha Bade amesema kuwa kutakuwa na maonesho kutoka jukwaa la mtandao, kushirikiana rasilimali, na lengo lake ni kuelimisha umma kuhusu haki za kijinsia na masuala ya haki za binadamu.
Aliyataja matukio mengine yatakayofanyika ni kama vile usiku wa Arusha ambapo kutatoa fursa ya kutosha kwa washiriki kufurahia kwa pamoja jiji la wa Arusha, kubadilishana mawazo na kujua tamadani zao, pia kutakuwa na mafunzo kuhusu masuala ya kijinsia katika shule za sekondari, kufungua rasmi klabu za haki za jinsia na washiriki watafurahia ziara kwenye maeneo maarufu ya kihistoria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo, ambaye ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sophia Wambura(katikati) na (kulia) ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Mbaraka Sehel(kulia) na kushoto ni Mwenyekiti Mwenyeji wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo, ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Aisha Bade.
Mwenyekiti Mwenyeji wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo, ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Aisha Zumo Bade(Kulia) akitaja matukio ya mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni