- Jaji Mkuu awaongoza waombolezaji
- Paroko ahimiza waombolezaji kujiandaa
Na FAUSTINE KAPAMA na
Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 20 Desemba, 2024 amewaongoza Watumishi
wa Mahakama ya Tanzania na waombolezaji wengine kumuaga Naibu Msajili, Mhe.
Maximillian Alphonce Malewo.
Mhe. Malewo, aliyefariki
Dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimili Mloganzila jijini Dar-es-Salaam tarehe
17 Desemba, 2024, ameagwa na watumishi wenzake nyumbani kwake Misugusugu Kongowe, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kabla ya mwili wake
kusafirishwa kuelekea Moshi, Kilimanjaro kwa mazishi.
Jaji Mkuu aliwasili
nyumbani kwa Marehemu majira ya saa 6.30 mchana na kupokelewa na Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, Mhe. Salma Maghimbi
aliyemwakilisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher
Mohamed Siyani.
Baada ya kuwasili katika
eneo la msiba, Mhe. Prof. Juma aliongozwa kwenda moja kwa moja kutoa heshima
zake za mwisho kwenye mwili wa Mhe. Malewo.
Ibada ya misa takatifu
ilifuata baada ya tukio hilo la kutoa heshima mwisho kabla ya kuwaruhusu
Viongozi wa Mahakama, ndugu na jamaa wa Marehemu Malewo kutoa salamu za pole.
Akiwasilisha salamu zake
kwa niaba ya Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki
Nkya amemwelezea Naibu Msajili Malewo kama mtumishi mcheshi na mwema
aliyetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili, uadilifu na weledi wa hali
ya juu.
Amesema Mahakama ya
Tanzania imepokea taarifa za msiba huo kwa mshituko mkubwa na ameacha alama
isiyofutika kutokana na uamuzi wake aliotoa na kwa jinsi alivyokuwa
anashirikiana na wenzake katika utendaji kazi.
Naye Paroko wa Parokia ya
Mtakatifu Policarp Misugusugu, Padri Venance Shiganga, akizungumza wakati wa
mahubiri kwenye ibada takatifu, amewaeleza waomboleaji wajitahidi kumjua mungu,
kumpenda, kumtumikia na mwisho kufika kwake mbinguni.
Amewasihi kila mmoja
kutafakari namna anavyoenenda katika maisha kama inavyompendeza Mungu, siyo kwa
kada ya sheria tu bali pia kwa kila mtu.
"Kila mmoja
ataondoka. Maisha ya duniani ni ya kupita, lakini unapitaje? Kila mtu anaogopa
kifo na tunaogopa kwa sababu hatujajiandaa. Kila mmoja atengeneze njia yake na
kujiandalia kifo chake. Kila mmoja ajiandae na kuishi maisha yanayompendeza
Mungu,"amesema.
Padri Shiganga,
aliyeshirikiana na Paroko wa Parokia ya Mbezi Luis, Padri Silyvester Msemwa
kuongoza ibada hiyo, amewaeleza waomboleza kuwa Mhe. Malewo ametutangulia,
hivyo kila mmoja tamwombee ili Mungu ampokee katika maisha yake ya milele na
wale ambao wamebaki wajitahidi kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Viongozi wengine wa
Mahakama waliohudhuria ibada hiyo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Lilian
Mashaka, Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Divisheni,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na Mahakimu mbalimbali.
Walikuwepo pia Wadau mbalimbali
wa Mahakama ya Tanzania, wakiwemo Mawakili wa Serikali na Mawakili wa
Kujitegemea, wananchi wa maeneo ya jirani na wengine wengi.
Mhe. Maximillian Alphonce
Malewo alizaliwa mnamo tarehe 28 Julai, 1975. Aliajiriwa na Mahakama ya
Tanzania tarehe 03 Januari, 2002 kama Hakimu Mkazi Daraja la III na kupangiwa
Kituo cha Kazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na kuhudumu katika wadhifa huo
hadi mwaka 2006.
Mnamo mwaka 2006 hadi
2009 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbinga. Mwaka
2009 aliteuliwa kuwa Naibu Msajili na kupangiwa Mahakama ya Rufani alipohudumu
hadi 2015.
Vilevile, akiwa
anaendelea na wadhifa wake wa Naibu Msajili, mwaka 2015 hadi 2016, Mhe. Malewo alipangiwa
kuhudumu Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na mwaka 2016 hadi 2021 alipangiwa
kuhudumu Mahakama Kuu Kanda ya Songea.
Aidha, mwaka 2021, Mhe. Malewo
alipangiwa kuhudumu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na mnamo Julai, 2024
alipangiwa kuhudumu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mpaka mauti
yalipomfika.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Naibu Msajili, Mhe. Maximillian Malewo aliyefariki Dunia tarehe 17 Desemba, jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Lilian Mashaka akitoa heshima zake za mwisho. Picha chini ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakitoa heshima zao za mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni