Jumanne, 11 Machi 2025

JAJI TIGANGA AANZA ZIARA YA UKAGUZI MKOANI SONGWE

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga ameanza ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama mkoani Songwe jana tarehe 10 Machi, 2025 akiwa anatarajia kukamilisha ziara hiyo ya ukaguzi mnamo tarehe 13 Machi, 2025. 

Akiongea na watumishi wa Mahakama mkoani humo Mhe. Tiganga amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuhakikisha lengo kuu la Mahakama linatimia kwa wananchi kupata haki zao kwa wakati bila mkwamo na manung’uniko yoyote, pia aliwapongeza watumishi hao kwa bidii kubwa wanazozifanya kuhakikisha wanatimiza jukumu lao utoaji haki kwa wananchi.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Mahakimu na watumishi wote kwa kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali uchache wenu. Pamoja na uchache wenu ni vyema tukafanya kazi kwa weledi, kujituma na kuwajibika kama ilivyo salamu yetu ya Mahakama na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati kwa wananchi kwani ndio lengo kuu la Mahakama,” alisema Jaji Tiganga 

Aidha, Mhe. Tiganga alitoa rai kwa watumishi hao, kuhakikisha kasi ya usikilizaji wa mashauri inaongezeka bila kuvunja sheria, taratibu, miongozo na kanuni ziliyowekwa ili kuongeza imani ya wananchi kwa Chombo chao cha utoaji haki nchini. 

Vilevile, katika ziara hiyo Mhe. Tiganga aliweza kutembelea Wilaya ya Mbozi na Momba na Mahakama zake za Mwanzo vituo vya Mlowo, Vwawa, Itaka, Kamsamba, Mkulwe, Chitete pamoja na mradi wa ujenzi wa Mahakama ya mwanzo Msangano na kujionea namna ujenzi unavyoendelea. 

Kwa upande mwingine ziara hiyo, itajumuisha pia Mahakama ya Wilaya Ileje pamoja na Mahakama zake za mwanzo, Mahakama ya Wilaya Songwe na Mahakama zake za mwanzo pamoja na mradi wa ujenzi wa Mahakama  ya mwanzo Wilaya ya Songwe Kituo cha Kanga na Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Katika ziara hiyo Jaji Tiganga ameambatana na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Emily Temu, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Francis Miti, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Francis Mwesiga Kishenyi, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi songwe Bw. Sostenes Mayoka, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya za Momba, Mbozi pamoja na Afisha utumishi na Afisa Tawala wa Mahakama za Wilaya Mbozi na Momba.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (watatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Momba.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akisaini katika kitabu cha wageni Mahakama ya mwanzo Itaba Wilaya ya Mbozi.

Naibu msajili Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda Mbeya Mhe. Aziza Temu (wa kwanza kulia), Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi Mavis Miti (katikati) na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa Songwe Mhe. Francis Mwesiga Kishenyi wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya ukaguzi Mahakama ya Mwanzo Kamsamba wilayani Momba. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akisalimiana na watumishi katika ziara yake Mahakama ya Mwanzo Kamsamba wilayani Momba.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akikagua ujenzi wa Mahakama ya mwanzo Msangano wilayani Momba mkoa wa Songwe.

Mtendaji wa kata ya Mkulwe Bw. Hakimu Bukuku (wapili kulia) akielezea changamoto mbalimbali wanazo kabiliana nazo na namna Mahakama inavyosaidia kuzitatua katika Kata hiyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbozi Mhe. Nemea Leon Chami akisoma taarifa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga wakati ziara hiyo.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni