• Ushiriki wa Wanawake kwenye fursa mbalimbali watajwa kuongezeka Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kigoma
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Emakulata Shuli aliwaongoza wanawake wa Mahakama Kanda ya Kigoma kujumuika na wanawake wenzao waliojitokeza wilayani Kibondo kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika Wilaya hiyo.
Mgeni Rasmi katika sherehe hizo zilizofanyika tarehe 08 Machi, 2025 katika viwanja vya Taifa Kibondo alikuwa Mkuu wa Wilaya Kibondo, Mhe. Agrey Magwaza aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye.
Akizungumza na wanawake waliofika katika viwanja hivyo, Mhe. Magwaza alisema kuwa, kupitia kauli mbiu isemayo kuwa “Wanawake na wasichana 2025; tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji” Serikali inasisitiza mambo kadhaa kwa jamii ili kuhakikisha kuwa jamii inastawi, ambapo alisema Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za kifedha inatoa mikopo nafuu kwa akina mama, kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi majumbani na kutoa fursa sawa za uongozi kwa wanawake katika ngazi mbalimbali.
Alisema kuwa, Serikali inashirikiana pia na Mashirika ya Kimataifa ili kuweka mazingira wezeshi ya kumuinua mwanamke kiuchumi kwani jumla ya makundi ya akina mama wajasiriamali 1,835 kwa kipindi cha mwaka 2024 sawa na asilimia 62 na kwa kipindi hicho Mkoa umetoa vitambulisho 1,119 sawa na asilimia 68 kwa wanawake, hata hivyo, alieleza kuwa, elimu ya ukatili wa kijinsia imeendelea kutolewa kwa wananchi mkoani Kigoma ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kutokomeza ukatili kwa akina mama na watoto.
Aliongeza kuwa, Serikali imetoa huduma kwa jumla ya manusura 3,319 wa ukatili ambapo kati ya idadi hiyo 3,253 sawa na asilimia 98 kuwa ni wanawake, imetajwa kuwa kiwango cha ukatili kwa wanawake ni kikubwa mkoani Kigoma, na kwamba bado haki za mwanamke zinakabiliwa na maadui wengi katika jamii kupitia wingi wa matukio hayo.
Alieleza kuwa, wahusika wa matukio mbalimbali ya ukatili mkoani humo wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa mjibu wa sheria za nchi ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii, hata hivyo alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwa na jamii inayokataa vitendo hivyo ambavyo ni adui kwa haki za wanawake na watoto katika nchi.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Zainabu Buyogela alisema kuwa, wanawake ni jeshi kubwa hivyo waungane kufichua uovu katika jamii, wachangamkie fursa za uongozi na ujasiriamali unaojitokeza katika maeneo yao, kukimbilia fursa za kifedha zinazotolewa na Serikali kupitia halmashauri zao.
Bi. Zainabu alitumia fursa hiyo kumshukuru mwanamke nambari moja Tanzania ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza nchi kwa haki na usawa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Abbas Rugwa aliwashukuru wanawake wa Mkoa huo kwa kujitokeza katika siku hiyo ya mwanamke duniani ambayo ni kwa ajili yao kupaza sauti juu ya masuala mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na kupinga vitendo vya kikatili na kutangaza fursa zilizopo kwa wanawake wenzao ambao bado hawajapata fursa za uongozi, kazi au ujasiriamali wa shughuli ndogondogo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Mhe. Aggrey Magwaza akihutubia umati wa wanawake waliojitokeza katika viwanja vya Taifa Wilaya ya Kibondo kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025.
Picha ya Watumishi Wanawake wa Mahakama wakipita mbele ya mgeni rasmi wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika viwanja vya Taifa Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma.
Bi. Pendo Elikado Evaristo akisoma risala kwa Mgeni rasmi, wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani zilizofanyika katika viwanja vya Taifa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni