Jumatatu, 10 Machi 2025

MSAJILI MKUU MAHAKAMA AUNGANA NA WATUMISHI WANAWAKE ARUSHA KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya ameungana na Watumishi Wanawake katika Mkoa wa Arusha kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08 Machi, 2025 kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid uliopo mkoani humo.

Maadhimisho hayo ambayo yaliwahuisha pia Watumishi Wanawake wa Mahakama Kanda ya Arusha yalianzia katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid na baadaye katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwakilishi wa Kampuni ya Utalii ya Thomson Safaris, Bi. Ruth Balele alisisitiza kuwa ni muhimu Wanawake kujitambua na kujithamini wenyewe kwanza katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa viwango vya hali ya juu ili jamii ijenge imani na akina Mama.

“Hiki sio kipindi cha kulalamika bali ni kipindi cha kuonesha kuwa sisi kama wanawake tunajitambua na tunaweza kufanya kazi zinazoonekana na zenye viwango vya hali ya juu. Ni muhimu mwanamke ajiamini na kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha anajitegemea na sio kuwa mzigo kwa mwanaume,” aliongeza Bi. Ruth.

Naye, Msaidizi wa Ofisi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bi. Upendo Dilunga akitoa mada ya Mwanamke na Saikolojia, alisisitiza kuwa, ni muhimu wanawake kuwafahamu wanawake wenzao kwamba ni wa aina gani ili iwe rahisi kujenga mahusiano rafiki na yenye faida katika maisha ya kila siku na hatimaye kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya alikabidhi keki kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta kwa watumishi hao pamoja na kufikisha salamu za pongezi na mafanikio katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulile Mwaseba na Mhe. Aisha Bade, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora pamoja na watumishi wa Mahakama katika Mkoa wa Arusha. Hafla hiyo, iliambatana pia na utoaji wa zawadi mbalimbali kwa watumishi.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalifanyika Kitaifa katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025 na Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2025 ni: “Wanawake na Wasichana, Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” inahimiza mamlaka mbalimbali kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata nafasi sawa ya kushiriki, kuendelezwa na kulindwa dhidi ya aina zote za unyanyasaji. Licha ya hatua kubwa zilizopigwa duniani kote, bado wanawake na wasichana wanakumbana na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa fursa na ubaguzi wa kijinsia.

Msajili wa Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (katikati) akimlisha keki Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento (kulia) wakati wa hafla fupi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025 katika viwanya vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya (kushoto) akikabidhi keki kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa pili kulia) wakati wa hafla fupi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa tarehe 08 Machi, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Monduli, Mhe. Pamela Meena (kulia) na wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento.

Mwakilishi wa Kampuni ya Utalii ya Thomson Safaris, Bi. Ruth Balele akizungumza wakati wa hafla fupi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025 iliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Msaidizi wa Ofisi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bi. Upendo Dilunga akizungumza wakati wa hafla fupi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Washiriki mbalimbali waliofika kuhudhuria hafla fupi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Watumishi wa Mahakama Arusha wakiburudika kwa kucheza muziki wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni