Jumanne, 25 Machi 2025

TUMIENI MVUA ZINAZOENDELEA KUPANDA MITI: JAJI RWIZILE

Na FESTO SANGA, Mahakama, Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Augustine Rwizile amewahimiza Watumishi wa Kanda hiyo kutumia vema fursa ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda miti ya matunda na kimvuli katika mazingira ya Mahakama.

Mhe. Rwizile alibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti mmomonyoko wa udongo, kukinga upepo mkali, kurejesha uoto uliopotea, kupendezesha Mahakama  na kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na mabadliliko ya tabia ya Nchi. 

Jaji Mgfawidhi alitoa wito huo katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama wa robo ya tatu ulioanza tarehe 20 Machi, 2025 alipotembelea Mahakama za Wilaya mpya na kupanda mti wa mfano ikiwa ni ishara ya kuongoza kampeni ya upandaji miti katika wilaya hizo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rwizile alipendezwa na namna Mahakama ya Wilaya Buhigwe walivyotekeleza azimio hilo. “Nawapongeza kwa kupanda miti, ila ongezeeni idadi katika maeneo yenu,” alisema Jaji Rwizile mara baada ya kutembelea Mahakama ya Buhigwe.

Hatua hiyo inafuatia baada ya azimio la kikao cha uongozi wa Mahakama cha Kanda hiyo kilichoketi tarehe 01 Machi, 2025 na kuazimia kuwa kila ziara za Viongozi na vikao vya Kanda vinavyofanyika kwa mzunguko kwa kila Wilaya katika maeneo husika kuwa na programu ya kupanda miti.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Fadhili Mbelwa, akitoa taarifa ya ukaguzi wa mashauri uliofanyika kwa njia ya mtandao, aliwapongeza Watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo kwa kufanya kazi kwa bidi, huku akiwahimiza kuendelea kusimamia mipango ya usikilizaji wa mashauri ili kya kujiepusha na mlundikano.

Alieleza kuwa siri ya kufanikiwa kumaliza mashauri na kuondokana na mlundikano ni pamoja na kuepuka kuahirisha mashauri kwa muda mrefu, kutopanga mashauri mengi kwa siku zaidi ya uwezo wa Hakimu wa kusikiliza mashahidi. Aidha, aliwafahamisha kuwa mafanikio ya kituo kwa umalizaji wa mashauri ndio hupelekea mafanikio ya Kanda kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Augustine Rwizile akipanda mti katika mazingira ya Mahakama ya Wilaya Kibondo. Pembeni ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe Maila Makonya.


 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akipanda mti aina ya Parachichi katika mazingira ya Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akipanda mti katika mazingira ya Mahakama ya Wilaya Uvinza. Pembeni ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe Misana Majula. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo. Kulia ni Mhe. Fadhili Mbelwa na kushoto ni Mhe. Maila Makonya. 

Mwonekano mzuri wa mazingira safi katika eneo la Mahakama.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni