Jumanne, 25 Machi 2025

WATUMISHI WA MAHAKAMA MASWA WATAKIWA KUDUMISHA MAADILI

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama - Simiyu

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wametakiwa kujiepusha na vitendo visivyo na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama hiyo jana tarehe 24 Machi, 2025 wakati wa ziara ya kawaida ya ukaguzi wa Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali amewataka watumishi wa Mahakama hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.

Mhe. Mahimbali aliwasisitiza watumishi wa Mahakama hiyo, hususani Mahakimu wapya walioajiriwa hivi karibuni kutokubali kuvunja heshima ya utu wao kwa kukubali kupokea kitu chochote kwa minajili ya kupindisha haki.

“Msiruhusu kuvunja utu wenu kwani una thamani kubwa sana ikilinganishwa na vitu mtakavyovipokea kwa muda mfupi ambavyo kimsingi vitaharibu thamani ya utu wenu,’’ alisema Jaji Mahimbali.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga kuhakikisha wanazingatia maadili kwa kufuata misingi ya utoaji haki sambamba na utoaji huduma bora kwa wateja wa Mahakama katika Kanda hiyo, huku akiwasisitiza kuwa, yeyote atakayefanya vitendo vya rushwa, atambue kuwa hakuna siri itakayoishi milele. 

“Tambueni kuwa, mkipokea rushwa, hakuna siri itakayoishi milele ni lazima mtabainika na hatua kali zitachukuliwa dhidi yenu, jiepusheni na tamaa za muda mfupi kwani kipato mnachokipata kutokana na kazi zenu si haba,’’ aliongeza Mhe. Mahimbali.

Hali kadhalika, Mhe. Mahimbali aliwataka watumishi wa Kanda hiyo kudumisha upendo, ushirikiano pamoja na kurithishana mambo mazuri ili kuzalisha viongozi wengine wazuri katika vizazi vijavyo ambapo alisema kuwa, hatua hiyo itaipa heshima kubwa Mahakama katika kuzalisha viongozi wenye maadili.

Katika hatua nyingine, Mhe Mahimbali alipata nafasi ya kutembelea Gereza la Malya lililopo wilayani Maswa Mkoani Simiyu ambapo alipata fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (katikati) akisisitiza jambo jana tarehe 24 Machi, 2025 wakati wa kikao na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa. Kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe Enos Misana (kushoto) akiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mhe. Aziz Khamis (kulia) wakisikiliza maelekezo ya Jaji Mfawidhi wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Mahimbali (hayupo katika picha) wakati wa kikao hicho.

Hakimu Mkazi, Mahakama ya Mwanzo Isanga Maswa, Mhe. Mbura Mjinja akifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Jaji Mfawidhi (hayupo katika picha).

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Wilaya Maswa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga pamoja na wa Gereza la Malya mara baada ya kumaliza shughuli za ukaguzi katika Gereza hilo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni