- Akipa kazi Chama cha Majaji na Mahakimu kuhusu upotoshaji
- Ataka upotoshaji mitandaoni ujibiwe kikamilifu
- Asema hakuna sehemu iliyo na haki kama Mahakama
Na FAUSTINE KAPAMA na
ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekitaka Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT)
kuandaa utaratibu wa kutoa ufafanuzi wa kweli kunapotokea upotoshaji wowote kwenye
mitandao ya kijamii kuhusu Mahakama na maamuzi yanayotolewa.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 15 Aprili, 2025 alipokuwa anafungua Mkutano Mkuu wa Mwaka
2024 wa JMAT, ambao unafanyika mwaka huu 2025 katika Hoteli ya Morena mjini
hapa.
‘Hili ni eneo ambalo
tunatakiwa tuliangalie kwa makini sana, kama JMAT tuwe na utayari wa kutoa
ufafanuzi wa kweli kama kuna upotoshaji wowote kuhusu Mahakama na maamuzi
yanayotolewa…
‘Tuwe na utaratibu wa
kujitokeza kama Chama, siyo kupotosha na sisi, bali kuelimisha. Kwa bahati
mbaya Wananchi wanategemea sana mitandao ya kijamii, wengine wanaamini. Kuna
upotoshaji mwingi sana,’ Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa moja ya upotoshwaji ambao unazunguka ni kwamba Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani wakiteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wanakuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa mujibu wa Katiba na
Sheria.
‘Sote tunafahamu hali
siyo hivyo kwani mara baada ya kuteuliwa huwa kuna kuapa kutekeleza majukumu
yako kwa mujibu wa Katiba na Sheria, bila chuki wala upendeleo…
‘Lakini ukisoma kwenye
mitandao, Wananchi wanaamimishwa kwamba unapoteuliwa na Rais unakuwa huna
uhuru. Hili jambo ni vizuri muwe mnalisemea mara kwa mara,’ amewaambia
wanachama wa JMAT.
Jaji Mkuu amefafanua kuwa
bahati nzuri hoja hiyo ilipelekwa kwenye Mahakama moja kule Canada na hoja kama
hizo zikatolewa kwenye kesi ya Matiko dhidi ya Barric Gold Cooperation na
uamuzi ulitolewa mwezi Oktoba 2024.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
kuwa katika uamuzi wake, Jaji wa Canada alitetea mfumo wa Sheria wa Tanzania na
kusema kuwa siyo kweli kuwa Rais anapoteua Majaji hachukui mamlaka yao
waliyopewa na kutoa maamuzi kwa mujibu wa Katiba ana Sheria.
‘Katika maamuzi hayo,
mfumo wa Katiba ya Tanzania umeweka kinga nyingi zaidi kuliko Katiba ya Canada
katika uteuzi wa Majaji. Hivyo, uhuru wetu wa kutoa maamuzi usiteteleshwe na
yale yanayoendelea kwenye mitandao, ni jukumu letu kuwaelimisha Wananchi, amesema.
Ameeleza pia kuwa bahati
mbaya huwezi kukuta kwenye mitandao ya kijamii watu wakijadili uamuzi huo kwa
sababu wapotoshaji hawataki Wananchi wajue ukweli.
Mhe. Prof. Juma amebainisha
kuwa hakuna sehemu iliyo na haki kama Mahakama kwani
Majaji na Mahakimu mara nyingi wamekuwa wakiwaongoza Wadaawa wanaofika mahakamani,
ambao hawafahamu taratibu, sheria na hawana Mawakili, namna ya kufanya
wanapotafuta haki.
‘Nadhani, Msajili Mkuu
tuweke takwimu ya Wananchi wangapi wanakuja mahakamani hawana msaada wowote wa
kisheria, lakini wanashinda na pengine wanashinda upande ule ambao wana
Mawakili,’ amesema.
Jaji Mkuu amesema kuwa mambo
kama hayo mazuri yanayofanyika mahakamani huwa hayatangazwi na Mahakama inaonekana
kama sehemu ambayo haina haki.
Akizungumzia uhuru wa
Mahakama, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa JMAT wana mchango mkubwa na moja ya
jukumu lao kwa mujibu wa Katiba yao ni kutetea uhuru wa Mahakama.
Amewakumbusha pia kwamba maendeleo
ya Teknolojia ya Habari yameongeza uwazi wa majukumu ya Majaji na Mahakimu na maendeleo
hayo makubwa yamekuja na changamoto dhidi ya Uhuru wa Mahakama.
‘Uhuru wa Majaji na
Mahakimu kuamua bila shinikizo hutikiswa sana katika zama hizi za
Mapinduzi ya Nne ya Viwanda kupitia mitandao ya kijamii,’Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Juma amebainisha
kuwa wapo watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wamejijengea umaarufu wa
kuweza kumshambulia Jaji au Hakimu yeyote kwa jina na kwa picha, na wafuasi
wake wakajazia maneno ambayo huwashushia heshima.
‘Ukiingia kwenye mitandao
ya kijamii unaweza kushangaa kama hii ni Tanzania ninayoifahamu au Tanzania ya
kufikirika. Ukweli mnaufahamu na nafikiri huu ukweli tuendeleaa kuutaja,’ Jaji
Mkuu amewaeleza wanachama wa JMAT.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni