Jumatano, 16 Aprili 2025

JMAT YAPATA SAFU MPYA YA UONGOZI

  • Naibu Msajili Elimo Massawe awa Rais

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kimefanya uchaguzi na kupata safu mpya ya uongozi katika ngazi mbalimbali, huku Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elimo Massawe akichaguliwa kuwa Rais wa Chama hicho.

Uchaguzi huo umefanyika jana usiku tarehe 15 Aprili, 2025 katika ukumbi wa hoteli ya Morena mkoani hapa, ukishuhudiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na Viongozi wengine.

Viongozi waliomaliza muda wao, Jaji John Kahyoza, Rais, Mhe. Shaibu Mzandah, Makamu wa Rais, Mhe. Lazaro Magai, Katibu. Mhe. Marry Kallomo, Naibu Katibu na Mweka Hazina, Mhe. Devotha Kasebele, wameshukuru kwa ushirikiano waliopata kwa wanachama.

Kabla ya kumaliza muda wao, Viongozi hao walipata nafasi ya kuzungumza na wanachama na kuwashukuru kwa ushirikiano wao kwa muda wote ambao walitumikia katika kipindi cha miaka minne.

Wakati wa uchaguzi huo, Mhe. Massawe ameibuka kidedea kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa chama hicho baada ya kupata kura 111, huku mpinzani wake wa karibu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Latifa Mansoor akijinyakulia kura 82, kati ya kura 280 zilizopigwa na wanachama wa chama hicho.

Mhe. Mansoor amepitishwa na wanachama wote kwa kura za ndiyo kuwa Makamu wa Rais mara baada ya kuwa mshindi wa pili katika kinyang`anyiro cha urais na wajumbe wote kuridhia kumpitisha kushika nafasi hiyo mara baada ya Rais kuwa na sifa ya Hakimu na mwenza wake kutakiwa kuwa Jaji kwa mujibu wa katiba ya JMAT.

Viongozi wengine waliochaguliwa ni Mhe. James Mniko aliyechaguliwa kuwa Katibu Mkuu kwa kura 80, Mhe. Teddy Raphael Mlimba aliyezoa kura 157 kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu na Mhe. Kasebele alifanikiwa kutetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 169 kati ya 280.

Akifunga mkutano huo, Mlezi wa Chama hicho na Jaji Mkuu wa Tanzania aliwapongeza washindi wote katika nafasi mbalimbali, huku akiwaahidi kuwapa ushirikiano na kuwaomba wasisite kwenda ofisini kwake kama watakumbana na changamoto yoyote.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifuatilia uchaguzi huo.

Wanachama wa kamati mbalimbali wakifuatilia uchaguzi wa Viongozi.

Wanachama wa JMAT wakipiga kura kuchagua Viongozi wapya-juu na picha mbili chini.




Mawakala wakihesabu kura za wagombea.

Makamu wa Rais, Mhe. Latifa Mansoor akitoa shukrani mara baada ya kupitishwa na mkutano mkuu.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni