Jumatano, 16 Aprili 2025

WASHIRIKI 15 WANOLEWA MAFUNZO YA UKATILI WA KINGONO

Na NAOMI KITONKA, Kituo Jumuishi Temeke

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amefungua mafunzo kuhusu Kuepuka Kutonesha Majeraha kwa Waathirika na Mashahidi wa Ukatili wa Kijinsia na Kingono (SGBV) yanayotolewa kwa Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka, na Maafisa Ustawi wa Jamii.

Akifungua mafunzo hayo tarehe 14 Aprili, 2025 yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama hiyo, Mhe. Mnyukwa alisisitiza umuhimu wa kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi, yenye huruma na inayowajali wahitaji wa huduma za haki hasa kutoka makundi yaliyo hatarini kama sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kukamilisha majukumu yake.

“Ukatili wa kijinsia umekuwa suala kubwa katika jamii yetu, hivyo ipo haja ya kuhakikisha haki inatendeka pale mashauri ya jinsi hiyo yanapoletwa mahakamani kwa kuzingatia hali walizo nazo wahanga wa ukatili huo na kama Mahakama na watu tuliopewa dhamana tunatambua umuhimu wa kutumia lugha yenye huruma, staha na weledi mkubwa pamoja na kujenga mazingira yenye usalama kwa waathirika wa ukatili tunaposikiliza mashauri mahakamani” alisema Mhe. Mnyukwa.

Jaji Mnyukwa alihimiza washiriki kuwa makini na mbinu wanazotumia katika kushughulikia mashahidi walio katika mazingira magumu ili wasiwajengee hali ya woga au kukumbuka majeraha yao ya awali.

Aidha, imeelezwa kuwa, mafunzo hayo yanatolewa kwa lengo la kuwajengea washiriki uwezo wa kuzuia na kuepusha kurejesha majeraha yatokanayo na ukatili wa kingono na kijinsia kwa ujumla wake na yamekusudiwa pia kubadilisha namna ya kuwachukulia na kuwalinda wale ambao wako hatarini katika michakato ya kisheria sambamba na usikivu wa Mahakama, kuchunguza mienendo tata ya unyanyasaji wa kijinsia na kuelewa jukumu muhimu ambalo Mahakama inatekeleza katika usimamizi wa haki.

Washiriki hao wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kujadili matukio halisi yanayotokea mahakamani wakati wa kusikiliza mashauri pamoja na kujifunza mbinu salama za kuwauliza maswali mashahidi walio katika mazingira magumu na kulinda haki na utu wa waathirika na jinsi ya kuwa  na mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa maarifa hayo muhimu katika kufanikisha zoezi la utoaji haki na pia kuwaepushia waathirika maumivu.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda na Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama IJA. Mhe. Husna Rweikiza.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na ‘Irish Rule of Law International’ (IRLI) na kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania yatafanyika kwa muda wa siku tatu. Yamehudhuriwa na washiriki mbalimbali wakiwemo Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyesimama) akitoa neno la ufunguzi mbele ya Washiriki wa mafunzo kuhusu Kuepuka Kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) yaliyofanyika tarehe 14 Aprili, 2025 kituoni hapo. Kulia ni Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe Husna Rweikiza, (kulia) na kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda.

Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akisisitiza jambo mbele ya washiriki wa mafunzo maalum kuhusu kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) yaliyofanyika tarehe 14 Aprili 2025 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

Washiriki wa mafunzo maalum kuhusu kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV), Mhe. Magdalena Malaba (kushoto) na Mhe. Juliana Nankoma (kulia) wakifuatilia kinachojiri katika mafunzo hayo.

Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Mhe. Husna Rweikiza akiwasilisha mada mbele ya washiriki wa mafunzo maalum kuhusu kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) yaliyofanyika jana tarehe 14 Aprili 2025 kituoni hapo.

Wajumbe wa Sekretarieti, Mhe. Edna Mollel na Mhe. Gloria Shuma wakifuatilia wasilisho la Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Husna Rweikiza (hayupo katika picha) katika mafunzo maalum kuhusu kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) yaliyofanyika tarehe 14 Aprili, 2025 kituoni hapo.

Washiriki wa mafunzo maalum kuhusu kuepuka utonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda (Hayupo pichani) yaliyofanyika jana tarehe 14 Aprili 2025 kituoni hapo.



Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akiwa katika picha ya pamoja washiriki wa mafunzo kutoka Ofisi ya Waendesha Mashtaka (NPS) waliohudhuria katika wa mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 14 Aprili, 2025 kituoni hapo.


Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo yanayohusu Kuepuka Kutonesha majeraha kwa waathirika na mashahidi wa ukatili wa kijinsia na kingono (SGBV) yaliyofanyika tarehe 14 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni