Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro
Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) jana tarehe 16 Aprili, 2025 kilifanya ziara ya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, iliyopo mkoani Morogoro katika kuendeleza mshikamano na uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa wanyamapori,
Ziara hiyo iliyoongozwa na Rais mpya wa Chama hicho, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elimo Massawe, ilikuwa sehemu ya shughuli za kuhitimisha Mkutano Mkuu wa JMAT uliokuwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali na kuchagua Viongozi wapya.
Akitoa neno la ukaribisho, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Msaidizi wa Hifadhi Augustine Massesa, alisema kuwa Mahakama na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ni wahifadhi wenza wa rasilimali za Taifa, kwa kuwa kila upande una silaha yake katika kulinda wanyamapori.
Kamishna Massesa alieleza kuwa ili kuimarisha uhifadhi, ni muhimu kwa Mahakama kuhakikisha kwamba pindi kesi zinazohusu uhalifu dhidi ya wanyamapori zinapopelekwa ziendeshwe kwa haraka, kwa usahihi na kwa kuzingatia ushahidi uliokusanywa.
Alisisitiza kuwa adhabu kali kwa kuzingatia sheria kwa wahalifu wa mazingira itasaidia kuwa mfano kwa wengine na kudhibiti uharibifu wa maliasili.
“Kila mtu ana silaha yake. Askari ana silaha ya moto, lakini ninyi Mahakama mna silaha ya sheria. Tunategemea kuona mnaendesha kesi kwa haki na kutoa adhabu kali kwa yeyote anayewadhuru wanyama wetu,” alisema Massesa.
Naye Afisa Hifadhi Mwandamizi Herman Bartazari, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utalii alitoa rai kwa Majaji na Mahakimu kutumia nafasi zao kama Viongozi kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria za uhifadhi na kuendesha magari kwa tahadhari wanapopita katika maeneo ya hifadhi.
“Madhara ya kutojali mazingira siyo tu kwa wanyama bali pia kwa kizazi chetu cha baadaye. Tusipotunza mazingira na wanyama, vizazi vyetu vitawaona kwenye vitabu tu,” alionya Bartazari.
Katika ziara hiyo, Majaji na Mahakimu walipata fursa ya kuona wanyama mbalimbali waliopo katika hifadhi hiyo na kupata elimu kuhusu changamoto za uhifadhi.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono kampeni ya Serikali ya kuhamasisha utalii wa ndani na kuchochea uzalendo katika kulinda rasilimali za Taifa.
Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Massesa (kushoto) akiwa pamoja na Rais mpya wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT), Mhe. Elimo Massawe pamoja na Viongozi wengine.
Viongozi mbalimbali pamoja na Majaji na Mahakimu wakipewa elimu ya mazingira na Wanyama.
Afisa Uhifadhi Mwandamizi Herman Bartazari akitoa elimu kwa Majaji na Mahakimu pamoja na Viongozi wengine.
Picha ya pamoja ya Majaji na Mahakimu pamoja na Viongozi wa Hifadhi ya Mikumi.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni