Jumatatu, 7 Aprili 2025

JAJI KAINDA AFUNGUA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA NYARAKA NA KUMBUKUMBU KIELEKTRONIKI

  • Lengo  ni kuwajengea uwezo Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama- Arusha

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na mgeni rasmi, Mhe. Sylvester Kainda amefungua mafunzo ya Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu kwa njia ya Kielektroniki ambayo yameanza kutolewa leo tarehe 07 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Akizungumza na Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Rufani, Masjala ndogo za Mahakama ya Rufani zilizopo katika Kanda mbalimbali na Zanzibar kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Kainda ameeleza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walengwa hao katika kutekeleza majukumu yao kwa kutumia mifumo ya kidigiti na hatimaye kutoa huduma bora za kimahakama kwa njia ya mtandao.

“Miongoni mwa maboresho ambayo Mahakama imeyafanya ni matumizi ya TEHAMA katika mifumo yake mbalimbali ya utoaji huduma kwa wananchi, hivyo matumizi ya Teknolojia yanalenga kuboresha utendaji kazi na ufanisi wa huduma tunazotoa,” alisisitiza Mhe. Kainda.

Katika maelezo ya awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kuwa, kwa sasa Mahakama inatumia mifumo mbalimbali ya kielektroniki kama vile mifumo ya uendeshaji mashauri, mifumo ya manunuzi na ya malipo na kadhalika.

Bi. Patricia ameongeza kwamba, ili mifumo hii na mingine itakayojengwa iweze kutumika vizuri, inahitaji Mahakama iwatayarishe watumishi wake kwa kuwapatia maarifa na ujuzi wa kuitumia, hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya kuwatayarisha na kuwawezesha watumishi kutumia mifumo hiyo ipasavyo.

Wasaidizi wa Kumbukumbu hao wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kuwa na uelewa mkubwa wa matumizi ya mifumo ya kidigiti ili kuwezesha Mahakama ya Rufani kuwa na watumishi wenye ujuzi zaidi wa namna ya kutekeleza majukumu yao kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.

Wawezeshaji katika Mafunzo hayo ni kutoka Chuo cha Upskill Training Institute cha Nairobi Kenya na mada mbalimbali zinazohusiana na Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu kwa njia ya Mtandao  zitafundishwa kwa njia ya vitendo zaidi ili walengwa waweze kupata maarifa yaliyokusudiwa.

Mafunzo hayo yatatolewa kwa kipindi cha wiki mbili kwa makundi mawili tofauti ya Wasaidizi wa Kumbukumbu kwa awamu ambapo jumla ya Wasaidizi wa Kumbukumbu 62 watanufaika na mafunzo hayo.

Ufunguzi wa mafunzo hayo, umehudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Sophia Massati na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bi. Asha Abdallah.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Sylvester Kainda akizungumza leo tarehe 07 Aprili, 2025 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC).



Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Rufani, Masjala ndogo za Mahakama ya Rufani zilizopo katika Kanda mbalimbali na Zanzibar wakipatiwa mafunzo ya Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu kwa njia ya kielectroniki yaliyoanza kufanyika leo tarehe 07 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mgeni rasmi katika Mafunzo ya Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu, Mhe. Sylvester Kainda (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha leo tarehe 07 Aprili, 2025.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Sylivester Kainda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu yaliyofanyika leo tarehe 07 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Walioketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Sophia Massati na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanznia, Bi. Patricia Ngungulu (kulia). Waliosimama ni wakufunzi wa mafunzo kutoka chuo cha Upskill Nairobi Kenya. (kushoto Kwenda kulia) Bw. Amos Kamau, Bi. Evelyn Mwihaki na Bw. Shadrack. Odondi. 

Mgeni rasmi katika Mafunzo ya Usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Sylvester Kainda (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo hayo yaliyoanza kufanyika leo tarehe 07 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa IJC Arusha. Walioketi ni kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Sophia Massati (kushoto) na kuia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Mahakama ya Tanznia, Bi. Patricia Ngungulu. Waliosimama ni Sekretarieti katika mafunzo hayo kutoka Makao Makuu ya Mahakama Dodoma. Kutoka kushoto ni Bw. Nazar Moshi, Bi. Doris Kaniki na Bw. Rajab Singana.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni