Na AMINA SAID, Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara
Mahakama
Kuu Divisheni ya Biashara imeendelea kuvuna mafanikio makubwa kupitia matumizi
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo Mfumo wa Usajili wa Taarifa za Wateja na Mawakili umeleta mapinduzi
katika utoaji wa huduma kwa wateja wa Mahakama hiyo.
Akizungumza
katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar
es Salaam, Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Edward Mbara, alieleza jinsi mfumo
huo unavyosaidia katika ufuatiliaji na uboreshaji wa huduma.
"Kwakuwa
mfumo huu unarekodi taarifa za wateja zikiwemo namba za simu, siku moja
nilipitia takwimu na kupata mteja mmoja aliyekaa mahakamani zaidi ya masaa Matano, nilimpigia simu kutaka kufahamu
kwanini alitumia muda mrefu, akanijibu kwamba alikuwa maktaba anajisomea
nyaraka mbalimbali," alisema Bw. Mbara.
Aidha,
aliongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuongeza ufanisi kwa kuwawezesha viongozi wa
Mahakama kufahamu kwa undani aina ya wateja wanaohudumiwa, jambo
linalorahisisha utoaji wa huduma bora na kwa wakati.
Katika kikao hicho, Mtendaji huyo aliweka bayana vipaumbele vya Mahakama hiyo kwa robo mwaka unaofuata, ambavyo ni pamoja na Kumaliza mashauri ya mlundikano, kuboresha na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) sambamba na kuwajengea uwezo watumishi juu ya matumizi ya mifumo Teknolojia.
Vipaumbele vingine ni kulipa stahiki za
watumishi na watoa huduma
pamoja na kufanya vikao vya kusukuma mashauri na vikao vya
utawala
Baraza
hilo pia lilihusisha uchaguzi wa Naibu Katibu wa Baraza la Wafanyakazi ambapo, Bi. Fullness Katekela na Bi. Tausi
Mwambujule walichuana kuwania nafasi hiyo. Katika uchaguzi huo ulioshirikisha
jumla ya wajumbe 21, Bi.
Fullness alipata kura 11
na Bi. Tausi
alipata kura 10. Hivyo,
Bi. Fullness Katekela alitangazwa mshindi na kuchukua nafasi ya Naibu Katibu wa
Baraza la Wafanyakazi
la Mahakama hiyo.
Mwenyekiti
wa kikao hicho ambaye ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Jaji Cyprian Mkeha aliwapongeza
Majaji kwa kazi kubwa ya kusikiliza na kuamua mashauri kwa kasi na ufanisi
mkubwa, hali iliyosaidia Mahakama hiyo kuendelea kuonesha mafanikio makubwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Baishara ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Cyprian Mkeha (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza jambo wakati wa kikao cha Baraza la Mahakama hiyo kilichofanyika hivi karibuni.
Afisa Utumishi Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara mmoja wa Wajumbe wa Baraza hilo, Bi. Adventina Kambuga akisisitiza jambo juu ya umuhimu wa kujiunga katika mfumo wa “PSSSF Kiganjani”.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakiimba wimbo wa mshikamano.
(Picha na ASHURA YUSUPH, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara)
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni