- Chatoka na maazimio kadhaa kuimarisha utendaji kazi
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Kikao cha siku mbili cha
Baraza la Wafanyakazi Taifa cha Mahakama ya Tanzania kilichokuwa kinafanyika
katika Ukumbi wa PSSSF jijini hapa kimehitimishwa leo tarehe 11 Aprili, 2025,
huku wajumbe wakitoka na maazimio kadhaa yanayolenga kuimarisha utendaji wa kazi.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha Kikao hicho, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma,
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo amewataka Viongozi kuanza mara moja
kutekeleza yale waliyojifunza wakati wa Kikao hicho.
Mhe. Prof. Juma
amesisitiza umuhimu wa Watumishi wa Mahakama kujiona kama sehemu ya Mahakama
licha ya kila mmoja kuwa na majukumu tofauti.
‘Tuna majukumu
mbalimbali, lakini wote tunafanya majukumu ya pamoja. Naomba Wafanyakazi wanaosaidia
au kufanikisha jukumu mama wasijione Watoto yatima kwa sababu wanafanya kazi
kubwa sana. Mahakama haiwezi kufanya kazi bila uwezeshaji unaofanywa na kada ya
Watumishi wengine,’ amesema.
Ameshukuru kwa maandalizi
mazuri ya shughuli mbalimbali za maandalizi zilizofanikisha Kikao hicho pamoja
na taarifa za utendaji kwenye maeneo kadhaa zilizowasilishwa na Viongozi wa
Mahakama.
Kadhalika, Jaji Mkuu
ameshukuru kwa mada nzuri zilizowasilishwa na wataalam kwenye maeneo mbalimbali
ambazo zimekuwa na manufaa makubwa kwa Watumishi wa umma.
Kabla ya kuhitimishwa kwa
Kikao hicho, wajumbe walipitishwa kwenye mada tatu muhimu, ikiwemo utaratibu na
maandalizi ya nyaraka kwa ajili ya mafao iliyowasilishwa na Meneja wa Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Victor
Kikoti.
Bw. Kikoti aliwaomba
wajumbe wa Baraza hilo kujaza kwa usahihi kumbukumbu za mafao na kuwasilisha
kwenye mamlaka husika madeni mapema, jambo litakalosaidia Mfuko kulipa mafao
kwa wakati.
Wajumbe pia walipokea
mada inayohusu maandalizi ya kustaafu katika utumishi wa umma iliyowasilishwa
na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. Venance Shilingi.
Dkt. Shilingi
aliwakumbusha wajumbe wa Baraza kuwa wasitegemee chanzo kimoja cha mapato na
kujiepusha na matumizi yasiyofaa ya fedha.
Kadhalika, wajumbe wa
Baraza walipokea mada inayohusu ulinganifu wa staili ya maisha namna mtumishi
anavyotakiwa kuishi kabla na baada ya kustaafu iliyowasilishwa na
Mwanasaikolojia maarufu, Bi. Sadaka Ahmed Gandi.
Maazimio yaliyofikiwa na
wajumbe wakati wa Kikao hicho yalikuwa nafasi ya Mahakama katika maandalizi ya
Dira ya Taifa 2050, kuwa Watumishi wote washiriki kikamilifu katika kutayarisha
mpango mkakati mpya wa Mahakama ambao utaendana na Dira hiyo.
Wajumbe pia wameazimia
kuwa kutokana na takwimu za mashauri za hivi karibuni kuonesha kuwa Mahakama za
Mwanzo zina asilimia 70 ya mashauri yote nchini, ipo haja ya kuweka mkazo zaidi
katika kuimarisha usimamizi wa utoaji haki katika Mahakama hizo ili kuongeza
ubora wa huduma ya utoaji haki katika ngazi hiyo.
Azimio jingine ni
Viongozi wa Mahakama kuendelea kufuatilia maslahi ya Watumishi na kwamba Kanda
za Mahakama ambazo hazijalipa posho ya mavazi kwa Wasaidizi wa Kumbukumbu,
Waandishi Waendesha Ofisi, Walinzi na Madereva zihakikishe zinalipa posho hizo
ifikapo Juni, 2025.
Wajumbe pia wameazimia
kuwa Mwajiri aangalie uwezekano wa kuongeza fedha katika michango ya Watumishi ili
waweze kupata huduma bora ya kiafya kupitia huduma za Bima ya Afya-NIHF.
Kadhalika, wajumbe wameazimia kuwa changamoto za kimfumo zinazoendelea kujitokeza na kubainishwa katika matumizi ya Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA-zitengenezewe rejesta maalum inayoainisha changamoto, ufuatiliaji na utatuzi ili kuleta ufanisi.
Sehemu nyingine ya nne ya Wajumbe wa Baraza-juu na chini- ikiwa kwenye kikao hicho.
Meneja kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya PSSSF, Bw. Victor Kikoti akiwasilisha mada kwenye Kikao cha Baraza hilo. Picha chini ni Mwanasaikolojia Maarufu, Bi. Sadaka Ahmed Gandi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni