Christopher Msagati – Mahakama, Manyara
Aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza
amekabidhi ofisi kwa Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Ilvin Mugeta jana tarehe 19 Juni,
2025 ikiwa ni baada ya kuhamishiwa Kituo kipya cha kazi cha Mahakama Kuu, Kanda
ya Shinyanga.
Mhe.
Mugeta ambaye kabla ya kuhamishiwa Manyara alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha. Katika hafla ya makabidhiano, Majaji hao
walipata wasaa wa kuzungumza na watumishi pamoja na wadau wa Mahakama, ambapo
Mhe. Kahyoza alitumia nafasi hiyo kuagana na Wanamanyara, huku Mhe. Mugeta
akatumia wasaa huo pia kujitambulisha na kwa watumishi wa Mahakama katika Kanda
hiyo.
Aidha,
akitoa shukrani wakati wa kuagana na watumishi, Mhe. Kahyoza alisema kuwa
ushirikiano alioupata toka Kanda ya Manyara usiishe mara baada ya kuondoka
kwake bali uendelee kwa Kiongozi huyo mpya na hata Viongozi wengine
watakaoendelea kuja kwenye Kanda hiyo.
“Leo
ni siku yangu ya pekee na adimu, nalazimika kuagana na watumishi niliokuwa nao
tangu mwaka 2022 ilipoanzishwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, watumishi hawa
wamenipa heshima kubwa sana. Viongozi hawawezi kufanya kazi peke yao isipokuwa
kwa ushirikiano na umoja wetu,” alisema Mhe. Kahyoza.
Naye,
Mhe. Mugeta alipokea kwa mikono miwili makaribisho aliyoyapata kwa watumishi wa
Kanda hiyo, huku akisisitiza kuwa ofisi yake ipo wazi kwa yeyote mwenye mawazo
ya kuboresha jukumu la msingi la utoaji haki. Alisisitiza kuwa yeye ni mtu wa
kazi na anavutiwa zaidi na wachapakazi.
“Nashukuru
kwa uongozi wa Mahakama kwa kuona kuwa mimi naweza kuendeleza kazi njema
iliyoanzishwa na Mhe. Kahyoza katika Kanda hii ya Manyara, kasi ya utendaji
kazi iliyokuwepo naamini tutaiendeleza na kushirikiana vema ili tuweze
kuwahudumia wananchi kwa namna ambayo inastahili,” alisema Mhe. Mugeta.
Kwa upande wake, akitoa
neno la shukrani kwa niaba ya watumishi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora alisema kuwa, wataendelea kutoa
ushirikiano kwa Kiongozi wao mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa. Vilevile Mhe. Kamuzora alimtakia majukumu mema Mhe. Kahyoza
katika majukumu yake anayokwenda kuyaanza katika Kituo chake Kipya cha Mahakama
Kuu Kanda ya Shinyanga.
Kauli hiyo iliungwa mkono
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Nenelwa Mwihambi pamoja na watumishi
ambao waliongeza kuwa wapo tayari kuyapokea maelekezo toka kwa Kiongozi huyo na
kuonesha ushirikiano.
Kwa namna ya pekee Wanamanyara watamkumbuka Mhe. Kahyoza kwa kuwa ndiye Jaji Mfawidhi wa Kwanza tangu kuanzishwa kwa huduma za Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara mnamo Mwezi Novemba mwaka 2022. Vilevile atakumbukwa kwa utaratibu aliouweka wa kusikiliza mashauri kwa wakati kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama za Mwanzo zilizopo katika kanda ya Manyara.
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta (kushoto) wakati wa makabidhiano ya kituo na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo Mhe. John Kahyoza (kulia) kufuatia uhamisho wa vituo vya kazi.
Mhe. John Kahyoza anayehamia Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga akisoma taarifa ya makabidhiano ya Mahakama Kuu Kanda ya Manyara mbele ya Jaji Mfawidhi Mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe Nenelwa Mwihambi pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara (hawapo pichani).
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Ilvin Mugeta ambaye ni Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara (wa sita Kushoto), Wengine ni Jaji Mfawidhi anayeondoka Manyara Mhe. John Kahyoza (wa sita kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora (wa tano kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa Mwihambi (wa tano kusho) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo (wa pili kushoto).
Jaji
Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta akisalimiana
na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara mara baada ya kuwasili Mahakamani hapo.
Bwana awabariki wote. Mhe, J i/c Kahyoza tunakutakia kila la kheri. Tutadumisha yote kwa weledi mkubwa. Mhe, J i/c Mugeta, karibu sana Kanda ya Manyara. Tunakuhahidi ushirikia mkubwa na kufanya kazi kwa weledi na kutekeleza maelekezo yako yote. Karibu sana .he, Jaji i/c Mugeka.
JibuFuta