Jumapili, 15 Juni 2025

JAJI MKUU WA SABA MZALENDO AAPISHWA

  •    Ni wa tisa katika historia ya Mahakama tangu kupata uhuru wa Tanzania
  •    Aahidi kuendelea kusimamia utoaji haki

 Na MARY GWERA, Mahakama- Dodoma

Leo tarehe 15 Juni, 2025 majira ya saa 4:10 asubuhi kwa mara nyingine historia ya Mahakama ya Tanzania imeandikwa kufuatia kuapishwa kwa Jaji Mkuu wa saba Mzalendo na wa tisa tangu kupata uhuru wa Tanzania ambaye ni Mhe. George Mcheche Masaju anayechukua nafasi ya mtangulizi wake, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyestaafu utumishi wa umma.

Mhe. Masaju ameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu- Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kumuapisha Jaji Mkuu mpya, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa, matarajio ya Watanzania ni kuona kuwa Mahakama inaendelea zaidi ya ilipo kwa sasa.

“Majengo, watenda kazi, mifumo na yote yaliyopo mahakamani yanahitaji kuendelezwa na Jaji Mkuu Mstaafu amesema vizuri kwamba, bado kuna miradi inaendelea, mingine fedha zake zipo, mingine fedha zake za kutafutwa lakini nikuhakikishie ushirikiano wa Serikali kwenye kukamilisha miradi hii,” amesema Rais Samia.

Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa, matarajio ya Watanzania pia ni kuona Mahakama inaendelea kusimamia haki ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo anatarajia kuwa jukumu hilo kubwa litasimamiwa vyema na Jaji Mkuu huyo.

“Katika kusimamia haki, Siku ya Sheria ya mwaka huu nilisema kuwa kazi yenu ni kusimamia haki. Kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu lakini kwa duniani kazi ya haki ni kazi ya Majaji, hivyo ni muhimu kusimamia haki kwa misingi tuliyojiwekea,” amesisitiza Rais Samia.

Ameongeza kuwa, Serikali itafanya kila linalowezekana kuendeleza ufanyaji kazi wa Mahakama kama alivyoahidi wakati analihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tarehe 22 Aprili, 2021 ambapo alisisitiza kuwa, Serikali itaendelea kufanya hivyo ili Mahakama ya Tanzania isimame vizuri na iwe ni moja katika Mihimili yenye hadhi duniani.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia ametoa rai kwa Jaji Mkuu mpya kuendelea na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai ili kuendelea na maboresho ya sekta ya sheria nchini.

“Nenda kaangalie ni maeneo gani tumetekeleza na ambayo bado hatujatekeleza na tuone jinsi tutakavyoendelea kuyatekeleza ili haki isimame vyema ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia huku akiongeza kwa kumpongeza Jaji Mkuu Mstaafu kwa kuhitimisha kazi hiyo bila makandokando.

Akizungumza baada ya uapisho, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumuona anafaa kushika nafasi hiyo ya kuongoza Mhimili wa Mahakama ya Tanzania.

“Ninachoweza kusema tu mbele yako Mheshimiwa ni kwamba, sisi kazi yetu Mhimili wa Mahakama ni kutoa haki na Katiba katika Ibara ya 107A na B imetueleza kanuni zinazotuongoza na sheria zote zinazotungwa huwa zina mambo matatu zinazungumza maslahi ya haki, maslahi ya umma na maslahi ya Taifa,” amesema Mhe. Masaju.

 Jaji Mkuu amesema kuwa, katika kutoa haki kuna kanuni ambazo ni mwongozo na mojawapo ya kanuni hizo ni kutenda haki kwa watu wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi na kijamii lakini pia kuharakisha utoaji haki isipokuwa kama kuna sababu ya msingi lakini pia kutofungwa na masharti ya kiufundi yanayoweza kusababisha haki kutotendeka kwa wakati.

Mhe. Masaju ameeleza kuwa, ataenda kushauriana na viongozi wenzake wa Mahakama ili kuona ni namna gani zaidi ya kuwafikia wananchi kwa kuwa Mahakama imelenga kuwasaidia wananchi (Citizen Centric Justice Service Delivery).

Amesema kuwa, ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, atajadiliana na wenzake kuona uwezekano wa kuwa na huduma za Mahakama ya Rufani kwa kila mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa haki.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah, Mawaziri, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama na Serikali.

Aidha, baada ya hafla ya uapisho, Jaji Mkuu mpya aliambatana na Jaji Mkuu Mstaafu hadi Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania iliyopo Mtaa wa Tambukareli jijini Dodoma ambapo alikaribishwa na watumishi wa Mahakama wakiongozwa na Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama.

Kadhalika, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemkabidhi rasmi Ofisi Jaji Mkuu mpya ambapo ameahidi kumpatia ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. George Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania leo tarehe 15 Juni, 2025 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akisaini hati ya kiapo mara baada ya kumuapisha Mhe. George Mcheche Masaju (hayupo katika picha) kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania leo tarehe 15 Juni, 2025 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (kulia) akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nafasi hiyo.


Jaji Mkuu mpya wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju.



Viongozi wa Serikali, Bunge na Mahakama pamoja na wageni wengine mbalimbali waliohudhuria katika hafla ya uapisho wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. George Mcheche Masaju.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akizungumza baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo leo tarehe 15 Juni, 2025 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati ) pamoja na Viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania (waliosimama).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (kushoto) na Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na watumishi wengine wa Mahakama alipowasili katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania baada ya kuapishwa rasmi leo tarehe 15 Juni, 2025 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Afisa Tawala wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Linda Lusajo (kushoto) akimkabidhi ua la pongeza Jaji Mkuuu mpya wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju wakati alipowasili katika viunga vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma mara baada ya hafla ya uapisho wake uliofanyika leo tarehe 15 Juni, 2025.

Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Lydia Luoga (kushoto) akimkabidhi ua Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kama ishara ya kumpongeza kwa kumaliza salama muda wake wa utumishi wa umma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na familia ya Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Wa pili kulia ni Mwenza wa Mhe. Prof. Juma, Bi. Marina Juma.



 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni