Na. Christopher Msagati- Mahakama, Manyara
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta amesisitiza upendo
miongoni mwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara. Mhe Mugeta
ameyasisitiza hayo alipokuwa katika ziara ya kuzifahamu Mahakama zilizopo
katika Mahakama Kuu Kanda ya Manyara hivi karibuni.
Katika
ziara hiyo, Mhe. Mugeta aliambatana na Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Kanda
ya Manyara ambao ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard
Mpepo, pamoja na Mtendaji wa Mahakama Bi. Nyanzobe Hemed.
Akiongea
na watumishi kwa nyakati tofauti katika vituo vyao Mhe. Mugeta aliwakumbusha
watumishi waendelee kufanya kazi kwa kupendana na kushirikiana ili kusaidiana
kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
“Hakuna
mtu ambaye ananufaika endapo atamchukia mtumishi mwenzake na kumfanyia visa
ambavyo vitamsababisha afukuzwe kazi, naomba mjue kuwa tunaishi kwa kutegemeana
kila mmoja. Kwa sababu hizo hatuna haja ya kuchukiana katika hizi kazi.
Nawasihi tupendane na kushirikiana vema na malengo yetu yatatimia ipasavyo”
alisema Mhe. Mugeta.
Aidha,
Mhe. Mugeta alipita katika Mahakama za Wilaya Mbulu, Hanang, Kiteto pamoja na
Simanjiro. Vile vile aliweza kupita katika Mahakama za Mwanzo Endagkot,
Dongobesh na Haydom zilizopo wilayani Mbulu pamoja na Mahakama za Mwanzo Bassotu
na Katesh zilizopo wilayani Hanang. Aidha, Mhe. Mugeta aliweza kukagua miradi
ya Ujenzi wa Mahakama zinazojengwa ambazo ni Mahakama za Wilaya Mbulu, Hanang,
Simanjiro pamoja na Mahakama ya Mwanzo Terrat iliyopo Wilayani Simanjiro.
Kwa
upande mwingine, Mhe. Mugeta aliweza kuwasisitiza watumishi kujikita katika
matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo kwa ubunifu ili kupata matokeo
yanayotarajiwa.
“Ni
kweli natambua changamoto ya uhaba wa bajeti pamoja na watumishi kwa kada
tofauti. Rasilimali hazijawahi kutosha hata siku moja popote pale, kwa
changamoto hii tuliyonayo inatupasa kuwa wabunifu na kutanguliza vipaumbele
katika utendaji kazi wetu na hapo ndipo tutafanikiwa” alisema Mhe. Mugeta.
Akisoma
Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro Mhe. Charles alimuomba Mhe. Mugeta
kuzungumza uongozi wa ngazi ya juu ili Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro wapate
majengo yanayojitosheleza kwa sababu hali ya Majengo iliyopo sasa hairidhishi.
“Mheshimiwa
Jaji, Wilaya yetu ya Simanjiro haina jengo hata moja ambalo linamilikiwa na
Mahakama, hivyo tunaomba ukatusemee katika ngazi za juu zaidi tupate majengo
yetu kwa sababu majengo yote yanayotumika sasa yameazimwa Serikali za Mitaa,
tunaona kuna juhudi za kumalizia ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya
Simanjiro lakini pia tunaomba Mahakama za Mwanzo pia zitazamwe” ilisema sehemu
ya taarifa hiyo.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Mugeta aliweza kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kiteto
ambapo alipokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Remidius
Mwema Emmanuel, ambaye aliahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika na Mahakama ya
Wilaya ya Kiteto kwa lengo la kutoa huduma zinazotakiwa kwa wananchi.
Hiyo
ni ziara ya kwanza iliyofanywa na Mhe. Mugeta katika kuzifahamu Mahakama
zilizopo katika Kanda ya Manyara tangu alipohamishiwa katika Kanda hiyo
akitokea Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na
aliyekuwa Jaji Mfawidhi Mhe. John Kahyoza ambaye alihamishiwa katika Mahakama Kuu
Kanda ya Shinyanga mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka 2025.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Simanjiro Mhe Charles Uisso akimtambulisha
mbele ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Manyara Mhe. Ilvin Mugeta alipofanya ziara Mahakamani hapo.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Manyara Mhe. Ilvin Mugeta akipokea maelezo juu ya hatua za mradi wa ujenzi wa
jengo la Mahakama ya Mwanzo Terrat wilayani Simanjiro kutoka kwa Msimamizi wa
mradi huo Mhandisi Magreth Kabepela anayeiwakilisha Kampuni ya Pioneer Builders
Company Ltd.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta (wa nne kushoto) Pamoja na msafara wake akiwa katika picha ya Pamoja
na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto alipofanya ziara Mahakamani hapo.
Hakimu
Mkazi Mahakama ya Mwanzo Haydom Mhe. Zena Mgalula (aliyenyoosha mikono)
akimuonesha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Manyara Mhe. Ilvin Mugeta Mazingira
ya Mahakama hiyo katika ziara iliyofanywa Mahakamani hapo. Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe Bernard Mpepo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu (hawapo pichani) alipokuwa katika ziara wilayani hapo. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe Bernard Mpepo, na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta (wa tatu kutoka kushoto) Pamoja na msafara wake akiwa katika picha ya Pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Bassotu iliyopo Wilayani Hanang alipofanya ziara Mahakamani hapo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang Mhe. Arnold Kileo akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mahakama hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta wakati wa ziara iliyofanywa Wilayani hapo.
Hongera sana Jaji i/c kwa ziara yako kwani kutembelewa na bosi ni faraja.
JibuFuta