Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mwenendo wa matumizi ya fedha za kuendeshea shughuli za Mahakama
imeelezwa kuwa, zitumike vema katika shughuli za Mahakama Kanda ya Kigoma
kupitia vipaumbele muhimu vilivyowekwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya
Tanzania (2020/2021-2024/2025) kwenye Nguzo ya Pili ya Mpango huo inayosema ‘Upatikanaji
na Utoaji Haki kwa wakati.’
Hayo yalibainishwa hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma wakati wa Kikao cha Bajeti ya Kanda ya Kigoma kilichoongozwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.
Akitoa neno la ufunguzi wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile alisema
kuwa, “Viongozi na Maafisa Bajeti wa Mahakama zote muhakikishe usikilizwaji wa
mashauri na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja
ukarabati wa Mahakama za mwanzo vinapewa kipaumbele zaidi katika bajeti zao ili
kuendana na Mpango wa maboresho ya Mahakama na usikilizwaji wa mashauri
sambamba na usimamizi wa haki za watumishi pamoja na kutunza samani za ofisi
zilizopo.”
Bw. Matotay aliwasisitiza wajumbe wa Kamati ya Bajeti kuwa
wabunifu katika kutekeleza bajeti zao zinazopatikana bila kutoka nje ya
utaratibu sahihi uliowekwa katika matumizi ya fedha za Serikali ili kuhakikisha
kazi za Mahakama yeyote hazikwami kwa namna yeyote ile.
Aidha, aliwasisitiza wajumbe wa kikao hicho kuhakikisha fedha za
mirathi zilizopo katika akaunti ya Mahakama zinalipwa kwa wadaawa na kwamba
imebainishwa kwamba zoezi la utambuzi wa fedha za mirathi unaendelea ili
kumaliza kabisa fedha za mirathi zilizopo katika akaunti ya Mahakama Kanda ya
Kigoma.
Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa aliwapongeza Maafisa Bajeti wa Mahakama za Wilaya
kwa taarifa nzuri za utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwani
imegusa vipaumbele vya Mahakam, imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa
usikilizwaji wa mashauri na utatuzi wa changamoto kutumia rasilimali fedha inayopatikana.
Mhe. Mbelwa alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Wilaya zote ndani ya Mkoa huo kuendelea kusimamia vema bajeti zao
ili zifanye shughuli muhimu za Mahakama kama Mpango Mkakati wa Mahakama huo
unavyoelekeza.
Wajumbe wa kikao hicho walikuwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya, Wakuu wa Idara za Mahakama Kuu Kigoma na Maafisa Tawala kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo, Uvinza, Kasulu, Buhigwe na Kakonko.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni