Jumanne, 28 Oktoba 2025

VIONGOZI WA MAHAKAMA KIGOMA WAKUTANA KUTATHIMINI NA KUJIPANGA KUBORESHA UTENDAJI KAZI WA KANDA

  • Wajipanga kushughulikia na kudhibiti mashauri ya mlundikano

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile ametoa rai kwa viongozi wa Mahakama za Wilaya zilizopo ndani ya Kanda hiyo kuongeza mikakati pamoja na ushirikiano katika uamuzi wa mashauri na kuzuia mashauri ya mlundikano sambamba na kuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali fedha zinazoletwa  kwa ajili ya kuendeshea shughuli za Mahakama.

Mhe. Rwizile alitoa rai hiyo tarehe 25 Oktoba 2025 katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Kigoma kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi cha Tathmini ya shughuli za Mahakama kwa robo ya pili ya mwaka kilicholenga kuweka mikakati wa kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2025/2026 hususani nguzo ya pili ya Upatikanaji na Utoaji Haki kwa wakati. 

Jaji Mfawidhi huyo vilevile, alitoa pongezi kwa juhudi za kila mtumishi katika eneo lake kwa kuwa na ushirikiano akieleza kuwa, ushirikiano ndio unaleta matokea mazuri ya utendaji. Aidha, pongezi zingine alizitoa kwa Mahakama za Wilaya Buhigwe na Uvinza kwa uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda na mbao na kuleta mandhari nzuri na hewa safi.

Aidha, aliongeza kusema, “tuongeze weledi wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao (virtual Court) ili kuhakikisha mashauri ya Ardhi, Benki na yale ya biashara yanasikilizwa na kumalizika mapema ipasavyo ikiwa ni sambamba na fedha za mirathi zilizopo katika akaunti ya mirathi zinalipwa kwa wanufaika kwa wakati.”

Pamoja na hayo, Mhe. Rwizile aliwaongoza Viongozi hao katika zoezi la upandaji miti Mahakama ya Wilaya Kigoma na kufanya mazoezi ya viungo ikiwa ni utamaduni wa Mahakama Kanda Kigoma ili kuimarisha afya za watumishi katika utendaji wa kila siku wa shughuli za Mahakama.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alisema, umeandaliwa mpango maalum wa kusikiliza mashauri yanayokaribia kuingia katika mlundikano na kuendelea kusimamia vizuri rasilimali zilizopo ili zilete tija na kuhakikisha inafikiwa ili kuendeleza mpango wa kuongeza vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani Kompyuta Mpakato.

Bw. Matotay alisema lengo la Kanda hiyo ni kuendeleza ushirikiano na wadau na kuimarisha maslahi ya watumishi na maadili ya kazi katika kuendeleza programu ya kupanda miti ya mbao na matunda katika maeneo ya majengo yote ya Mahakama Kanda ya Kigoma na kukamilisha programu ya Mahakama bila matumizi ya karatasi (Paperless Court).

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alisema kuwa, Mahakimu Wakazi Wafawidhi waainishe maeneo ambayo watumishi na wadau wa Mahakama wanaweza kupewa mafunzo ya ndani katika kuboresha shughuli za Mahakama pamoja na Kwenda na  na kasi ya usikilizwaji wa mashauri mapema ipasavyo na kwa njia ya Mahakama Mtandao.

Hata hivyo, Mhe. Mbelwa aliwakumbusha Wafawidhi hao kuongeza usimamizi katika eneo la mashauri ili kuzuia mlundikano wa mashauri katika vituo vyao.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho walikuwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya mkoani Kigoma, Wakuu wa Idara za Mahakama Kuu Kigoma na Maafisa Tawala kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo,  Uvinza, Kasulu, Buhigwe na  Kakonko.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo hivi karibuni wakati wa Kikao cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Wajumbe wa kikao wakifuatilia kwa makini taarifa ya utendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma wakati wa Kikao cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay akifafanua jambo kwa msisitizo wakati wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akipanda mti wa mchikichi katika eneo la wazi lililopo Mahakama ya Wilaya Kigoma mara baada ya kumaliza cha kikao cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika  hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akipanda mti wa mchikichi katika eneo la wazi lililopo Mahakama ya Wilaya Kigoma mara baada ya kumaliza kikao  cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika  hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa kikao  cha Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, (kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili  Mbelwa  na wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na waliosimama ni wajumbe wengine wa kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni