- Msajili Mahakama Kuu aeleza umuhimu wa wajumbe kwenye kikao hicho
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Kamati ya Kitaifa ya
Kusukuma Mashauri ya Jinai leo tarehe 27 Octoba, 2025 imefanya kikao kujadili
mambo mbalimbali yanayolenga kuharakisha usikilizaji na utoaji haki kwa wakati
kwenye mashauri ya jinai.
Kikao hicho ambacho
kimefanyika katika moja ya kumbi za mikutano katika Jengo la Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma kimeongozwa na Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.
Wajumbe kutoka Taasisi
mbalimbali, ikiwemo Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka,
Magereza, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Chama cha
Mawakili Tanganyika na nyingine zinazounda Kamati hiyo wamehudhuria kikako hicho
muhimu.
Wakati wa Kikao hicho,
wajumbe hao wamejadili mambo mbalimbali, ikiwemo taarifa ya hali ya mashauri ya
mlundikano mpaka kufikia mwezi Septemba, 2025, hali ya Mahabusu magerezani na
mkakati wa kupunguza mlundikano.
Akizungunza wakati wa
kufungua kikao hicho, Mhe. Tengwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
aliwaeleza wajumbe hao kuwa ni muhimu katika kuhakikisha haki jinai
inasimamiwana inatekelezwa na kwamba kila mmoja wao ana jukumu ambalo
utekelezaji wake unategemea mwenzake.
Amesema kuwa vikao hivyo
vya kusukuma mashauri ambavyo vinafanyika mara kwa mara ni zaidi ya jukwaa na
lengo lake kuu ni kubaini changamoto ambazo zinaweza kuathiri utendaji kazi
wao.
‘Iwapo mmoja wetu kwenye
mnyororo huu atapatwa na changamoto, utendaji wa mwenzake utaathirika. Ni
ukweli usiopingika kwamba kila mmoja ana jukumu lake, lakini hii haimaanishi
kwamba kila mwenye jukumu anajua maarifa na ukweli wote...
‘Tunapokuwa tunakuta hivi tunapata wasaa wa kusikiliza changamoto mbalimbali zinazomkabili kila mmoja na wote kwa pamoja tunaweka mikakati ya pamoja ya namna gani ya kuitatua kwa sababu wote tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba haki inatendeka,’ Mhe. Tengwa amesema.
Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai, Mhe. Elimo Masawe [kulia] akiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati wa kikao.
Wajumbe wa Kamati hiyo
wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.
Sehemu nyingine ya
wajumbe wa Kamati wakiwa katika ukumbi wa mkutano.
Wajumbe wa Kamati-juu na
chini- wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kikao.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni