Jumatatu, 27 Oktoba 2025

MAHAKAMA MOROGORO YAFANYA MAFUNZO KWA MAHAKIMU

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro

Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, tarehe 23 na 24 Oktoba, 2025 iliendesha mafunzo ya kitaaluma kwa Mahakimu wa ngazi zote wa Kanda hiyo ili kuongeza uelewa na kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa sheria na kufanikisha usikilizaji wa mashauri mapema ipasavyo.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Cate Hotel mkoani hapa yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda y Morogoro, Mhe, Rose Ebrahim.

Mhe. Ebrahim alieleza kuwa kuwepo kwa mafunzo hayo kulitokana na uhitaji ulioanishwa na Mahakimu na Wadau wa haki katika Wilaya zote katika Kanda hiyo.

Alisema kuwa ilikuwa muhimu kwa Mahakimu kuwezeshwa kwenye eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA], hasa ikizingatia kuwa Mahakama za Mwanzo walianza kuchapa mienendo ya mashauri moja kwa moja kwenye kompyuta mpakato na kuachana na matumizi ya majalada magumu tangu mwezi Aprili ,2025.

Hatua hiyo iliwezesha maudhui ya mafunzo hayo kuwa “Kuboresha ufanisi wa Mahakama na maendeleo endelevu kupitia uelewa wa mageuzi ya kisheria kuimarisha utaalamu wa kitaaluma, ujumuishaji wa akili bandia na usawa kati ya kazi na maisha.”

Wawezeshaji wa mafunzo hayo walikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga aliyewasilisha mada kuhusu ‘Utekelezaji wa Umuazi na Amri za Mahakama’ na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi aliyezungumzia ‘Matumizi ya Akili Bandia Mahakamani AI’.

Wengine na mada zao kwenye mabano ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba (Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai na Madai pamoja na Makosa yanayojitokeza mara kwa mara) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe (Utekelezaji wa Tuzo na Amri za Mahakama pamoja na Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi).

Watoa mada wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo (Uongozi wa Kimkakati na Sifa za Kiongozi), Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Simon Swai (Uendeshaji wa Mashauri ya Mirathi na Taratibu Sahihi za Kufunga Mirathi) na Daktari wa Saikolojia ya Afya ya Akili, Dkt. Chris Mauki [Afya ya Akili na Elimu ya Kijamii].

Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Mahakimu wameshukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro na kuahidi kutumia ujuzi waliojengewa kwa siku hizo mbili katika kuleta ufanisi na upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim (katikati), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Hadija Kinyaka (wa pili kulia),  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, Mhe. Elimo Masawe (wa kwanza kulia), na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni (wa kwanza kushoto) wakiwa katika mafunzo hayo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu  Dodoma, Mhe. Elimo Masawe, akitoa elimu kwa Mahakimu hao.

 

Mahakimu wakifatilia mafunzo mbalimbali yaliyokuwa yanatolewa.

 

Daktari wa Saikolojia ya Afya ya Akili, Dkt. Chris Mauki akitoa mafunzo juu ya saikolojia wa afya ya akili, tabia na mahusiano ya kijamii.

 

Mahakimu wakifuatilia mafunzo ya akili mnemba (AI).

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

 

 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni