Ijumaa, 17 Oktoba 2025

KUTENDA HAKI NDIO MSINGI WA TAIFA

  • Kaimu Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu wamtaka Hakimu mpya kumtegemea Mungu
  • Wasisitiza haki huinua Taifa

 Na HABIBA MBARUKU – Mahakama Dodoma.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, kwa nyakati tofauti wamesisitiza watumishi wa Mahakama kumtegemea Mungu katika utendaji haki, uwajibikaji na kujituma bila kujali mazingira ili kuendelea kusimamia haki katika maeneo ya kazi.

Viongozi hao wametoa wito huo leo tarehe 17 Octoba, 2025 katika hafla ya uapisho wa Hakimu Mkazi mpya, Mhe. Hillary Massala Kuzenza iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya uapisho huo, Mhe. Kagomba amemtaka Hakimu huyo kumtegemea Mungu katika kutekeleza majukumu yake, huku akizingatia uadilifu, uaminifu na kujituma. Amemuhimiza kujitoa kufanya kazi mahali popote nchini bila kujali changamoto za kimazingira, jambo ambalo litaendelea kumpa uzoefu, ujasiri na kujituma katika kazi.

“Kubwa katika yote ambayo nadhani niseme, kama kurejea katika msisitizo ni kuendelea kumtegemea Mungu katika kazi tunayofanya. Tunatambua kwamba kazi ya kuhukumu ni kazi yake na sisi ambao tumekasimiwa hapa duniani tunaofanya kwa niaba yake tunapaswa kufanya kwa matarajio yake yeye aliyetuleta hapa,” amesema Kaimu Jaji Kiongozi.

Aidha, Mhe. Kagomba amemshauri Hakimu huyo kuchangamkia fursa halali atakazozikuta katika maeneo atakayopangiwa kazi ikiwa ni pamoja na fursa za kilimo, biashara, uvuvi na ufugaji  ili kujiendeleza kiuchumi, hasa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Wako Watumishi ambao watakwenda Kigoma na utawakuta wamenuna na kukasirika, lakini wakiondolewa huko watanuna na kukasirika pia baada ya kugundua kuwa kuna fursa, kuna kilimo na biashara. Nakushauri kuwa ukijiingiza kwenye biashara utaona changamoto nyingi, lakini kilimo au uvuvi  ni shughuli ambazo hazina migogoro,” amesema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel amemtaka Hakimu Mkazi huyo kuzingatia haki katika utendaji kazi, huku akisisitiza kuwa, haki huinua Taifa na kwamba nchi isiyosimamia haki huporomoka.

“Mara zote haki huinua Taifa na haki isipotendeka nchi huanguka na nchi ambayo haisimamii haki kwa kweli ni changamoto,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.


Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba akizungumza jambo mara baada ya hafla ya Uapisho wa Hakimu Mkazi mpya, Mhe. Hillary Massala Kuzenza (hayupo katika picha) leo tarehe 17 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Hakimu Mkazi mpya, Mhe. Hillary Massala Kuzenza akisikiliza kwa makini mawaidha/wosia kutoka kwa Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba (hayupo katika).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno kwa Hakimu Mkazi mpya, Mhe. Hillary Massala Kuzenza aliyeapishwa leo na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha)


Picha ya Uapisho: Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimuapisha Hakimu Mkazi mpya, 
Mhe. Hillary Massala Kuzenza leo tarehe 17 Oktoba, 2025  kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni