Jumatano, 15 Oktoba 2025

MAHAKAMA KUU KAZI YAKABIDHI JUZUU ZA MAAMUZI CHUO CHA USTAWI WA JAMII

Na Mwandishi Wetu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, tarehe 10 Oktoba 2025, amekabidhi Juzuu za Maamuzi ya Migogoro ya Kazi kwa Chuo cha Ustawi wa Jamii.

Mhe. Dkt. Mlyambina alikabidhi nakala mbili (2) za Juzuu za Maamuzi ya Migogoro ya Kazi Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na nakala sabini (70) za Labour Court Case Digest, akiwa ameambatana na mahakimu wa Mahakama Kuu.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Jaji Dkt. Mlyambina amesema kuwa kuleta Juzuu hizo Chuo cha Ustawi wa Jamii ni heshima ya kutambua mchango na kazi inayofanywa na Chuo cha Ustawi wa Jamii, ambacho ni Chuo pekee nchini kinachotoa taaluma za kazi na kuzalisha maafisa wanaokwenda kufanya kazi katika Mahakama za kazi kama wasuluhishi na watatuzi wa migogoro ya ajira.

Aidha, Juzuu hizo zimepokelewa na Naibu Mkuu wa Chuo - Fedha na Utawala, Dkt. Eventus Mugyabuso, kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho.

Kadhalika Juzuu za Maamuzi ya Migogoro ya Kazi zinahusu kesi zilizotolewa maamuzi kuanzia mwaka 2010 hadi 2024, na zinatarajiwa kusaidia wanafunzi, wanazuoni wa sheria na watafiti kupata rejea sahihi na kuelewa mwenendo wa tafsiri za kisheria katika migogoro ya ajira nchini.

Kwa Upande wake Naibu Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Eventus Mugyabuso amemshukuru Jaji Mlyambina kwa kuona umuhimu wa kuleta Juzuu hizo chuoni hapo ambazo zitaongeza ujuzi kwa wanafunzi wa Taaluma za kazi na wanazuoni kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (wa tatu kushoto) akikabidhi Juzuu za Maamuzi ya Migogoro ya Kazi kwa Chuo cha Ustawi wa Jamii.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (kulia) akiteta jambo na Naibu Mkuu wa Chuo - Fedha na Utawala, Dkt. Eventus Mugyabuso
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Divisheni ya Kazi mara baada ya kukabidhi Juzuu za Maamuzi ya migogoro ya kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Mkuu wa Chuo - Fedha na Utawala, Dkt. Eventus Mugyabuso.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Cassian Matembei akiwa na sehemu ya watumishi wa Mahakama hiyo.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni