Jumatano, 15 Oktoba 2025

MWILI WA MAREHEMU FREDRICK BINAMUNGU KAKURWA WAAGWA KWA IBADA MAALUM

Na. Rehema Awet – Mahakama, Mwanza

Mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa aliyekuwa Hakimu Mkazi II Mahakama ya Mwanzo Nyanchenche umeagwa tarehe 13 Oktoba, 2025 nyumbani kwake maeneo ya Kabwalo Buswelu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Ibada ya kuaga mwili wa marehemu ilihudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Mhe. Winifrida Beatrice Korosso, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na viongozi mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Mwanza.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Mwanza, Bw. Tutubi Deo Mangazeni alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mahakama na kuwapa pole wafiwa wote wakiwemo familia, ndugu jamaa marafiki na wafanyakazi wenzake waliohudhuria ibada ya kuaga mwili wa marehemu.

Aidha, kwa masikitiko makubwa alieleza namna ambavyo Mahakama imepata pengo kwa kuondokewa na mfanyakazi wake ambaye alikuwa kijana hodari na mchapakazi.

Vilevile, alieleza kuwa Mahakama kama mwajiri ilivyoshiriki katika taratibu zote za kuhifadhi na hatimaye kuusafirisha mwili wa marehemu kwa ajili ya kuupumzisha kwenye nyumba yake ya milele huko kijijini kwao ambapo mazishi yamepangwa kufanyika mnamo tarehe 14 Octoba, 2025

Baada ya ibada ya kuaga mwili wa marehemu, ulisafirishwa kuelekea kijijini kwao Bundaza Kata ya Nyakibimbili mkoani Kagera.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Bw.Tutubi Deo Mangazeni akiaga mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa.

Sehemu ya Majaji, Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania wakishiriki Ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa, kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Winifrida Beatrice Korosso akiwaongoza Majaji wenzake Mhe. Penterine Kente na Mhe. Amour Khamis, wengine ni Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, Mhe. Kassim Robert, Mhe. Emmanuel Ngigwana na Mhe. Kamana Kamana, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Janeth Musaroche na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza Mhe. Erick Marley 

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Winifrida Beatrice Korosso akiaga mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Kamana S Kamana akiaga mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa.

Sehemu ya waombolezaji na watumishi wa Mahakama Kanda ya Mwanza wakishiriki kuaga mwili wa marehemu Fredrick Binamungu Kakurwa.




 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni