Jumanne, 14 Oktoba 2025

TANZIA; NAIBU MSAJILI MAHAKAMA KUU KANDA YA SHINYANGA, MHE. ASHA MWETINDWA AFARIKI DUNIA


 Aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Marehemu Mhe. Asha Khamis Mwetindwa enzi za uhai wake.

                                                 TANZIA

Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake, aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Asha Khamis Mwetindwa kilichotokea leo tarehe 14 Oktoba, 2025 Saa 1 asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bw. Bakari Mketo, Marehemu Asha Mwetindwa alianza kujisikia vibaya wiki moja iliyopita ambapo alianza kupata matibabu katika Hospitali za Kolandoto Shinyanga na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Bw. Mketo amesema kuwa, baadaye Marehemu Mhe. Asha Mwetindwa alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma mpaka alipofikwa na umauti.

Mtendaji huyo amebainisha kwamba, kwa sasa taratibu za mazishi zinaendelea kuratibiwa na taarifa kamili itatolewa mara baada ya kukamilisha taratibu.

Marehemu Asha Mwetindwa aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania tarehe 6 Juni, 2007 kama Hakimu Mkazi Daraja la II na amewahi kufanya kazi katika Wilaya za Lindi na Singida.

Aidha, marehemu Mwetindwa aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama za Wilaya za Masasi na Muleba na mwaka 2022 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga.

Mwaka 2023 Marehemu Asha Mwetindwa aliteuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na kupangiwa Kituo cha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga nafasi aliyoitumikia hadi umauti ulipomkuta.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba huo mzito wa kuondokewa na Mpendwa wetu.

HAKIKA SISI SOTE NI WA MWENYEZI MUNGU NA KWAKE YEYE TUTAREJEA (INNA LILLAH WA INNA ILLAH RAJIUN). 

 

 


1.    

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni