Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jumla ya Wanafunzi nane wa Kidato cha nne kutoka Shule ya
Sekondari Buteko iliyopo mkoani Kigoma wamefanya Kazi Mradi (Project) yenye
mada isemayo ‘Nini changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutoa
haki kwa wananchi’ ikiwa ni mchakato wa kuhitimisha masomo yao katika ngazi
hiyo ya masomo.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano akishirikiana na Msaidizi
wa Sheria wa Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Valerian Msola walitoa elimu kwa
wanafunzi hao waliofika mahakamani hapo tarehe 10 Oktoba, 2025 ili kufahamu kuhusu shughuli mbalimbali na nafasi ya Mahakama katika kutoa haki
kwa wananchi.
Mhe. Galiatano aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, Mahakama inatoa
haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba hujikita katika usahihi wa shauri
lililopo mbele ya Mahakama husika ili kuhakikisha kila anayefikishwa au kufika
mahakamani anapata haki yake mapema ipasavyo na bila upendeleo wa aina yoyote.
Alisema kwamba, zipo changamoto kadhaa ambazo Mahakama inakutana
nazo inapotekeleza wajibu wake wa kutoa haki ambapo alisema, “Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni changamoto kwa sasa, kwakuwa Mahakama mtandao
inahitaji vifaa na mtandao imara katika kuendesha mashauri Mahakamani, hivyo
wadau wanaoshirikiana na Mahakama wanapokuwa hawana mtandao imara husababisha
kukwama kwa usikilizwaji wa mashauri Mahakamani.”
Hata hivyo aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, uelewa mdogo wa matumizi
ya Mahakama Mtandao kwa wananchi
umechangia pakubwa changamoto ya kitehama, kwani kwa sasa Mahakama inafanya
shughuli zake zote kwa mtandao.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Kanda hiyo, Mhe.
Valerian Msola alisema kuwa, Mahakama ni kati ya Mihimili mitatu ya Dola kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatimiza wajibu wake
kisheria na ni Chombo pekee chenye mamla ya utoaji haki nchini, hivyo ina
wajibu wa kutoa haki bila kuacha shaka.
Aidha, Mhe. Msola aliwataka wanafunzi wasome kwa bidii ili
wafikapo katika ngazi ya elimu ya juu waweze kusoma Sheria na baadaye waweze
kuwa Wanasheria wazuri na wenye maadili katika kuhudumia jamii ya Watanzania.
Aliongeza kwa kuwaomba wanafunzi hao kuendelea kuipenda
Mahakama na kwamba elimu waliyopata waipeleke katika jamii wanayoishi ili jamii
ifahamu kuwa Mahakama ndio chombo pekee kinachotoa haki bila upendeleo wowote.
Kwa upande wake Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bi. Amina Husein
aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa kuridhia wao kuja
kujifunza mambo mengi ya Mahakama na umuhimu wa Mahakama katika jamii ya
Watanzania.
Msaidizi wa sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Valerian Msola (katikati) na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano, (kulia) pamoja na Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma , Bi. Happiness Elia wakiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Buteko mkoani Kigoma waliotembelea Mahakama Kuu Kigoma tarehe 10 Oktoba, 2025 kwa ajili ya kufanya Kazi Mradi (Project) yenye mada isemayo ‘Nini changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutoa haki kwa wananchi.’
Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano akisisitiza jambo wakati alipokuwa akitoa elimu kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Buteko iliyopo mkoani Kigoma.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akiwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Buteko jinsi Mahakama huketi wakati wa kusikiliza mashauri.
Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bi. Amina Husein akiuliza swali la kutaka kufahamu changamoto ambazo Mahakama inakabiliana nayo kwa sasa katika usikilizaji mashauri na utoaji hukumu.
Mwanafunzi Bi. Sania Yenga Msabaha, aliyevutiwa kukalia kiti cha mamlaka ya Mahakama mara baada ya kusema kuwa yeye anayo nia ya kuwa Hakimu na hatimaye Jaji.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni