Jumatatu, 13 Oktoba 2025

MBEYA YAFANYA KIKAO CHA MENEJIMENTI YA KANDA

Na. Muksini Nakuvamba-Mahakama, Mbeya

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Said Kalunde ameongoza kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Mbeya inayojumuisha mikoa ya Mbeya na Songwe shughuli hiyo ilichofanyika tarehe 09 Oktoba, 2025 Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.

Akiwasilisha taarifa ya utawala na ushughulikiaji wa mashauri kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 kwa Mahakama za Mkoa wa Mbeya Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Wilaya Rungwe Bw. Alintula Ngalile alifafanua kuwa taarifa hiyo inaainisha uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali, utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati.

Taarifa hiyo pia, ilieleza maendeleo ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA, hali ya majengo, viwanja na miradi ya maendeleo inayoendelea katika mkoa wa Mbeya pamoja na ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa elimu kwa umma na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika mnyororo wa utoaji haki.

Vilevile, taarifa hiyo ilieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, changamoto pamoja na mikakati waliyojiwekea katika kupambana na chanagamoto hizo.

Afisa Utumishi huyo akatoa shukurani “Mhe. Mwenyekiti tunashukuru kwa uongozi wako ambao unasisitiza katika uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia uweledi, kanuni na taratibu katika utumishi wa Umma, ili kufanikisha haya yote msisitizo mkubwa unawekwa kwa watumishi na viongozi kuwa waadilifu wakati wa kutekeleza wajibu wao kiuweledi na kufanya kazi kwa umoja.”alisema Bw. Ngalile.

Aidha, iliwasilishwa taarifa ya kiutendaji na usimamizi wa mashauri katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa Mahakama za Mkoa wa Songwe.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Bw. Sostenes mayoka, alifafanua hali ya rasilimali watu, usimamizi wa rasilimali fedha, hali ya majengo, viwanja na miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Songwe, vyombo vya usafiri hali ya mashauri na ziara za kutembelea Magereza Wilaya ya Mbozi na Ileje.  

Aidha, taarifa hiyo pia ilieleza mafanikio, changamoto, mikakati waliyojiwekea katika kupambana na chanagamoto hizo na mipango ya baadae

“Tuna mipango kazi ya baadae ikiwemo kuanza zoezi la kupima maeneo yote ya viwanja vinavyomilikiwa na Mahakama za Mkoa wa Songwe ili kupata hati. Pia tunalenga kupunguza mlundikano wa mahabusu katika magereza yetu kwa kupunguza masharti ya dhamana ili wale wanaodhaminika waweze kuwekewa dhamana.” alisema Bw. Mayoka.

Aidha, taarifa za mirathi na malipo ya mirathi ilikuwa sehemu ya utekelezaji ikimtaka kila Hakimu wa Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe aliwasilisha taarifa za Mirathi kwenye wilaya yake.

Kwa upande wa Mahakama za Mkoa wa Mbeya taarifa ya jumla kuhusu malipo ya mirathi kwa Mahakama zote za Mkoa wa Mbeya iliyowasilishwa na Msaidizi wa Hesabu Mahakama Kuu Mbeya Bw. Nassir Upete.

Mhe. Kalunde akatoa shukurani kwa wajumbe wote kwa kushiriki na kusisitiza kuwa, viongozi wawe na desturi ya kushirikisha watumishi wa chini katika kujadili mambo mbalimbali ya kiofisi ili kuboresha utendaji kazi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde (Kulia) akiongoza kikao cha Menejimenti Kanda ya Mbeya, Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti.

Sehemu ya wajumbe wa menejimenti kanda ya Mbeya

Afisa Utumishi Mwandamizi (wa kwanza kushoto) akiwasilisha taarifa ya kiutendaji na ushughulikiaji wa mashauri kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 kwa Mahakama za Mkoa wa Mbeya.

Msaidizi wa Hesabu Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bw. Nassir Upete akiwasilisha taarifa ya mirathi katika kikao hicho

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe  Bw. Sostenes Mayoka (kulia) akiwasilisha taarifa ya utawala na uendeshaji wa mashauri kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 kwa Mahakama za Mkoa wa songwe.

Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama ya wilaya Mbozi Mhe. Nemes Chami akiwasilisha taarifa za Mirathi Mahakama ya Wilaya ya Mbozi -Songwe.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni