- Vikao vya maandalizi vikihusisha wadau vyaanza
Na EUNICE LUGIANA-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, jana tarehe 16 Octoba,
2025 imefanya kikao na Watendaji Wakuu wa Taasisi mbalimbali kujadili namna bora
ya kushiriki kwenye Wiki ya Usuluhishi itakayofunguliwa tarehe 20 Novemba, 2025
jijini Dodoma.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Banki Kuu ya
Tanzania jijini Dar es Salaam kilifunguliwa na Amidi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Iman Aboud, ambaye alimwakilisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mhe. Aboud alisema kuwa japokuwa jukumu
kubwa la Mahakama ni kutenda haki mapema ipasavyo, lazima kuzingatia njia
mbadala au utatuzi mbadala wa migogoro ambao umesisitizwa katika Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Ibara ya 107 (d).
Alisema kuwa kwakuwa Mahakama imedhamiria kwa dhati kuona masuala ya
utoaji wa haki yanapaswa kufanywa mapema ipaswavyo, hatua hiyo ni mwendelezo
katika kukamilisha jukumu kubwa iliyopewa kikatiba la kutoa haki.
Mhe. Aboud alieleza kuwa kikao hicho kina lengo la kujadili utatuzi
mbadala wa migogoro, njia ambayo itasaidia kwa upande wa Mahakama kupunguza
mashauri ambayo yasingekuwa na ulazima wa kufika mahakamani iwapo wadau husika kwenye
Taasisi au Ofisi zao wangeitumia.
Alisisistiza kwamba njia mbadala ya utatuzi wa migogoro ni rahisi, haina
gharama na huwafanya pande zote mbili kuwa na mahusiano mazuri. “Hii ni njia
ambayo inatakiwa tuienzi na kuhakikisha tunaitafutia mikakati bora ya kuitumia,”
alisema Jaji Abood.
Kadhalika, alibainisha kuwa njia hiyo itawavutia wawekezaji kuja
kuwekeza Tanzania maana watajua migogoro ya kibishara haichukui muda mrefu
kuisha na baadaye kuendelea na biashara kwa amani kwakuwa wafanyabishara wengi
hawapendi migogoro.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra
Maruma alisema kuwa mkutano huo unaweka historia ya safari ya kuhamasisha
matumizi ya njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro nchini Tanzania.
Alisema kuwa lengo kuu la Mahakama na wadau wake ni kupata uelewa wa pamoja
juu ya kuhamasisha usuluhishi wenye kuleta ufanisi na tija, siyo tu kama inavyotajwa
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali hata kwenye Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025- 2050.
Alibainisha kuwa nchi nyingi duniani hivi sasa zimekuwa zikitumia njia za
usuluhishi na kuondokana na dhana ya kuendesha mashauri mahakamani kwa muda
mrefu na hii ni kutokana na faida nyingi zinazotokana na njia hiyo.
Akitoa takwimu za migogoro katika Kituo hicho, Mhe. Maruma alisema wameshudia
ongezeko kubwa katika kutatua migogoro. ‘Takwimu zinaashiria nia njema kwamba
tukiendelea kwa juhudi za pamoja tunaweza kufanikisha sana migogoro mingi
ikaishia kwenye hatua za usuluhishi,’ alisema.
Alisema kuwa mwaka 2023 migogoro 82 ilifanikiwa kupitia njia ya
usuluhishi, kwa mwaka 2024 migogoro 109 na mpaka Oktoba 2025, migogoro 70
imemalizika kwa njia hiyo.
Naye Prof. Zakayo Lukumai, akitoa taarifa ya hali ya usuluhishi Tanzania,
alisema kuwa usuluhishi uliingizwa mahakamani kama kiambata (court annex
mediation) na kuanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye
Mahakama Kuu na sasa imeenea Mahakama zote.
Alieleza kuwa kwa sasa somo la usuluhishi limeingizwa kwenye mitaala ya Shule
ya Sheria kwa Vitendo na linafundishwa kwa vitendo. Mhe. Lukumau alisema kuwa kuanzishwa
kwa Kituo cha Usuluhishi kumeongeza kasi kwa njia mbadala kuweza kukubalika
katika utatuzi wa migogoro.
Prof Lukumai alitoa wito kwa Vyuo Vikuu nchi kulifanya somo hilo kuwa la
lazima ili kuanza kujenga misingi tangu mwanzo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi wa Mabenki, Taasisi za Usuluhishi na vitengo vyote vinavyoshughulika na usuluhishi.
Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud [juu na chini] akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni