Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi jana tarehe 15 Februari, 2026 aliwaongoza watumishi wanawake wa Kanda hiyo kutoa msaada wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Sekondari Pugu iliyoko jijini Dar es Salaam.
Akizungumza akiwa ofisini kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Mhe. Maghimbi alieleza dhumuni la wao kufika shuleni hapo kuwa ni matokeo ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika mwaka jana 2025 na wao kama wanawake watumishi wa Mahakama Kanda ya Dar es salaam walikuwa na vitu ambavyo wao waliwiwa kuvitoa kwa wanafunzi hao lakini baada ya kuvitoa waliomba wapewe mahitaji ya msingi yanayohitajika kwa wanafunzi hao.
Jaji Maghimbi alisema baada ya kupata mahitaji hayo, watumishi wanawake wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam walichanga pesa ili kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo na pia waliwashirikisha baadhi ya wanaume ambao waliguswa nao walichangia na hivyo kuweza kupatikana kwa mahitaji yote yaliyohitajika.
Aliongeza kuwa, kama kinamama watumishi wa Mahakama Kanda ya Dar es salaam wameomba mahusiano ya karibu na shule hiyo na chochote kitakachotokea wameomba kuwasiliana ili kwa kile watakachoweza kusaidia wasaidie.
Akizungumzia kuhusu taarifa ya Mwalimu Msuya, Mhe. Maghimbi alisema siku zote yeye amekuwa akifikiri kuwa ana msongo wa kazi anayoifanya lakini alipomsikiliza Mwalimu Msuya na kazi ya kuhudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum, alikiri kwamba amepata nguvu mpya ya kufanya kazi na ameona kazi yake haina msongo kama ilivyo ya walimu hao, “kama unafikiri una tatizo fikiri tena,” alisema Mhe. Maghimbi kwa msisitizo.
Aidha, akizungumza na wanafunzi wenye mahitaji maalum, Jaji Maghimbi aliwaeleza dhumuni la safari hiyo na kusema kwamba baada ya kutembelea kwa mara ya kwanza waliona kwamba wanatakiwa kufanya nacho kazi kwa ukaribu kutokana na mioyo yao na wala sio mfumo wa kazi yao.
Aidha, aliwapongeza wanafunzi hao kwa matokeo mazuri katika mitihani yao na kuwaambia kuwa wao wameonesha kuwa chochote kinawezekana kwa sababu wanao uwezo wa kufanya vitu, kwakuwa uwezo wa kufikiria na kuelewa kile kinachofanyika na kuwa makini na kuwasihi kuwa na moyo huo pasipo kuteteleka.
Akizungumzia kuhusu Mchepuo mpya ulioanzishwa shuleni hapo wa Sanaa kwa Masomo ya Historia, Lugha ya Kiingereza na Jiografia, Mhe. Maghimbi aliwatia moyo kuwa, hayo sio masomo wa wanawake kama wanavyofikiria bali ni masomo yanasomwa na wanaume pia.
Aliongeza kuwa, kutokana na kuanzishwa kwa mchepuo huo kuna uwezekano mkubwa wa kuwapata Wanasheria, Majaji na Mahakimu na hivyo Mhe. Maghimbi ametoa mwaliko maalum kwa Wanafunzi wa masomo hayo kutembelea Mahakama na kuona shughuli za kimahakama zinavyoendeshwa.
Kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Jaji Maghimbi alipata wasaa wa kupata historia fupi ya Shule hiyo kutoka kwa Makamu Mkuu wa Shule Taaluma, Mwalimu Juma Msuya ambapo alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1948 ikiitwa Mtakatifu Francis ikiwa chini ya Kanisa Katoliki na kwamba baada ya kupata uhuru ilibinafsishwa na kuitwa Pugu na ilianza na jumla ya Wanafunzi nane (8) na mpaka sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1000 wa Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita.
Mwalimu Msuya alisema kati ya wanafunzi hao wapo Watoto wenye mahitaji maalum kuanzia mwaka 1990 Serikali ilipoingia Mkataba wa Elimu Jumuishi ndipo shule hiyo ilitakiwa kupokea Watoto wenye mahitaji maalum haswa wale wa viungo ingawa kwa sasa wanachukua mchanganyiko wale wenye uziwi hafifu, mgongo wazi hasa wale wenye vichwa vikubwa.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa, mwanzo Watoto hao walikuwa hawafanyi vizuri darasani lakini kwa bahati nzuri Serikali imeajiri Walimu wenye elimu maalum ambao wamepambana mpaka sasa wamefanikiwa kufuta daraja sifuri (division zero) na hata daraja la nne (division four). Matokeo ya juzi kulikuwa na Watoto 24 lakini hakuna aliyetoka daraja la tatu wala la nne.
“Watoto utakapowaona na ukiangalia na mafanikio wanayoyafanya ndipo utakapoamini ‘disability is not inability’ kwamba kutokana na ulemavu alionao basi anashindwa kila kitu hapana ni pale wanapowezeshwa basi na wenyewe wanaweza,” alieleza Mwalimu Msuya.
Mwalimu huyo alisema kuwa, kuna baadhi ya Wanafunzi hao hawawezi kuandika hivyo wanapata usaidizi wa notisi na ndio maana wameomba mashine za kuchapia na kurudufu. Na kuna baadhi wanatumia kompyuta ambazo kuna baadhi wamepatiwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa kutoa maoni na maombi ya mahitaji mengine Mwanafunzi aliyejulikana kwa jina maarufu Bangimoto alisema anachukizwa na tabia ya baadhi ya watu wenye ulemavu kukaa barabarani na kuomba badala ya kujishughulisha na kupata kipato halali.
Mwanafunzi huyo aliongea kwa uchungu na kuonyesha namna gani walemavu wanachukuliwa na jamii kutokana na wao mwenyewe kuubeba udhaifu.
Vitu vilivyokabidhiwa katika ziara hiyo ni pamoja na mashine mbili za kisasa cha kuchapa zenye skana na kurudufu, karatasi katoni 40, wino sita (6), flashi za hizo mashine, mashuka tisa, Madaftari (Counter books) seti mbili, ‘diapers’ katoni mbili, sabuni za unga, kipande na za kuogea, mafuta kwa ajili ya watu wenye changamoto ya Ngozi (albino) na vitu vingine vingi pamoja na vinywaji baridi ambavyo vimegharimu jumla ya fedha za Kitanzania 5,564,000/=.
Katika ziara hiyo ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Maghimbi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Ubungo, Mhe. Tumsifu Barnabas na Kigamboni Mhe. Mwanakombo Athuman, Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Tuikailize, Msaidizi wa Kumbukumbu, Mwandishi Mwendesha Ofisi pamoja na Madereva.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akikabidhi vifaa vya Shule kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Sekondari Pugu walipotembelea shule hiyo hivi karibu kwa lengo la kutoa msaada kwa wanafunzi hao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo (kushoto), Makamu Mkuu wa Shule Utawala (kulia), Mwalimu Ndimwangwa Nzota.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni