Jumatatu, 16 Februari 2026

'USULUHISHI NI SUALA LINALOHITAJI UVUMILIVU NA USIKILIZAJI WA UMAKINI'

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma ametoa rai kwa Wasuluhishi nchini kuwa wavumilivu na kusikiliza kwa makini wakati wanapofanya usuluhishi.

Mhe. Maruma aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu ya Upatanishi kwa Mahakimu na Wasajili wa Kanda ya Dar es Salaam yaliyofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke.

Jaji Maruma alisema, endapo Msuluhishi ana haraka, hana uvumilivu na hana usikivu hawezi kufanya usuluhishi na kwamba kama Msuluhishi akiwa hana usikivu na uvumilivu hata wale anaowasuluhisha hawawezi kumuamini, wadaawa wakimuangalia msuluhishi wanajua tu kwamba anawajali na kuwasikiliza ama la.

Ameongeza kuwa, uvumilivu na utulivu unasababisha usuluhishi, hivyo kuwataka kuwa wavumilivu hata kama wadaawa watawashambulia kwa maneno makali wao wawe chanya na wavumilie hatua hiyo itasababisha wadaawa kurudi kwenye mstari, hivyo usuluhishi kuendelea na kufanikiwa.

Awali akifungua mafunzo hayo, Mhe. Maruma alieleza kuwa, mafunzo hayo ni mwendelezo wa juhudi za Mahakama katika kuwajengea uwezo watumishi wake ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Jaji Maruma alisema mafunzo hayo, yanafanyika wakati muafaka na muhimu sana wakati Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 inahimiza usuluhishi kama nyenzo  muhimu ya msingi  mkuu katika kuleta amani, umoja na utulivu  katika Taifa letu.

“Hii inaendana na mikakati ya Mahakama  katika kukuza matumizi ya usuluhishi ili kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo  kama inavyosisitizwa  katika ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisisitiza.

Aidha Mhe. Maruma afafanua kwamba Mahakama zinaendelea kukabiliwa na ongezeko la mashauri ambayo mengi kati yake yanaweza kutatuliwa kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa maridhiano bila kupita mchakato mrefu wa mashauri ya shauri la kawaida hivyo kuokoa gharama na muda ambao utatumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alisema kuwa, upatanishi wa Mahakama umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwezesha migogoro kumalizika kwa haraka na kwa sasa ongezeko la upatanishi limezidi asilimia 50 tofauti na hali ilivyokuwa miaka minne nyuma.

“Hali hii inatupa matumaini na chachu ya kuendelea kuwajengea uwezo Mahakimu na wadau wa usuluhishi ili kuongeza ufanisi katika kutatua migogoro kupitia upatanishi na kufika malengo yaliyopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 ya kutumia njia hii katika kuleta  amani na utulivu katika jamii zetu,” alisema Jaji Maruma.

Aliongeza kwamba, mafunzo hayo ni maandalizi ya Wiki ya Usuluhishi ambayo imepangwa kufanyika mwezi Machi nchini kote na kusema kuwa mafunzo hayo ni mwanzo wa mafunzo ambayo yataendelea kutolewa kwa Majaji, Mahakimu na Wadau ili kujenga uwezo wa ufanisi wa kutekeleza njia ya upatanishi katika kuharakisha upatikanaji wa haki.

Kadhalika alisema kwamba, ushiriki wa Majaji, Mahakimu, Wasajili na wadau wa Taasisi nyingine unaonesha kuwa, usuluhishi si jukumu la mtu mmoja bali ni juhudi ya pamoja ya taasisi zote zinazohusika na utoaji haki. Majaji na Mahakimu ingawa si Wasuluhishi katika mashauri yao, ni wasimamizi na walezi wa mchakato wa usuluhishi, hivyo ni muhimu kuwa na uelewa wa kina wa msingi, taratibu na falsafa ya usuluhishi.

Naye Naibu Msajili ya Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi Mhe.Augustina Mmbando alisema, Usuluhishi huimarisha  upatikanaji wa haki mapema ipasavyo, kwa gharama nafuu na kwa kuzingatia mahusiano ya kijamii na kibiashara.

Mhe. Mmbando alisema usuluhishi sio mbadala wa Mahakama bali ni nyenzo inayosaidia Mahakama kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kwa mtazamo unaomjali binadamu.

Akizungumzia kuhusu miongoni mwa Wadau waliohudhuria mafunzo hayo ambao ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Mhe. Mmbando alisema uwepo wa TIRA katika mafunzo hayo una umuhimu wa pekee kwa kuwa Sekta ya Bima ni miongoni mwa sekta zinazozalisha migogoro mingi ya kibiashara na kimikataba ambayo kwa asili yake inafaa kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi.

Aliongeza kuwa, ushirikiano kati ya Mahakama na Taasisi za Udhibiti kama TIRA ni nguzo muhimu katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa haraka, haki na kwa namna inayohifadhi mahusiano na kuimarisha imani ya wadau katika mfumo wa haki.

Naye Mwezeshaji katika mafunzo hayo Mhe. Mhangwa Yunge alisema usuluhishi ni mzuri kwakuwa unaokoa muda na pia Wadaawa wanabaki na amani na kuongeza kuwa sio kila mgogoro unaweza kusuluhishwa bali kuna migogoro mingine wahusika wanakuwa hawako tayari kusuluhishwa.

Mafunzo hayo yaliwezeshwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Angela Bahati na Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi (IJC) Temeke, Mhe. Mhangwa Yunge.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Naibu wasajili, Mahakimu, Wadau na Mtendaji wa Mahakamu Kuu Kituo cha Usuluhishi, Bi. Hellen Mkumbwa.

 Jaji  Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma akifundisha mada wakati wa Mafunzo yaliyotolewa hivi karibuni kwa Wasuluhishi wa Mahakama.


Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi (IJC) Temeke na Mwezeshaji wa Mafunzo kwa Wasuluhishi wa Mahakama, Mhe. Mhangwa Yunge akiwaongoza washiriki wa mafunzo hayo kuimba wimbo uliotungwa wakati wa mafunzo hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi na Mwezeshaji wa Mafunzo (kulia), Mhe. Angela Bahati Salema na Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi (IJC) Temeke na Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Mhe. Mhangwa Yunge wakisikiliza michango iliyokuwa ikitolewa na washiriki wa mafunzo hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu Kituo cha usuluhishi na mwezeshaji wa mafunzo, Mhe. Angela Bahati Salema (kulia) akipokea cheti katika hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi (IJC) Temeke na Mwezeshaji wa Mafunzo ya Upatanishi, Mhe. Mhangwa Yunge akipokea cheti katika hafla ya kufunga mafunzo hayo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbado  akipokea cha ushiriki wa mafunzo katika hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni