Na DHILLON UISSO-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto [IJA], hivi karibuni kiliendesha mafunzo ya siku tatu yanayohusu ya upataniishi
wa Mahakama ili kuimarisha uwezo wa kutumia njia ya upatanishi
ambayo ni rafiki katika utatuzi wa migogoro.
Mafunzo hayo ya siku
tatu yaliyoanza tarehe 11 Februari, 2026, yakiwaleta pamoja Mahakimu wa ngazi
zote pamoja na Naibu Wasajili kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na
Divisheni, yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi,
Mhe. Zahra Maruma.
Akizunzungumza kwenye
ufunguzi huo, Mhe. Maruma alieleza kuwa mafunzo hayo yamefanyika
katika wakati muafaka na muhimu wakati dira ya 2050 inahimiza usuluhishi kama nyenzo muhimu ya
msingi mkuu katika kuleta amani, umoja na utulivu katika taifa letu.
‘Hii inaendana na
mikakati ya Mahakama katika kukuza matumizi ya usuluhishi ili kuharakisha
upatikanaji wa haki mapema ipasavyo kama inavyosistizwa katika ibara ya 107A
(2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ alisema.
Jaji Mfawidhi
alibainisha kuwa mafunzo hayo pia ni moja ya maandalizi ya Wiki ya Usuliuhishi
ambayo imepangwa kufanyika mwezi Machi 2026 nchini kote, hivyo, ni mwanzo wa
mafunzo ambayo yataendelewa kutolewa kwa Majaji, Mahakimu na Wadau ili kujenga
uwezo wa ufanisi wa kutekeleza njia hiyo ya upatanishi katika kuharakisha
upatikanaji wa haki.
Mhe. Maruma
alibainisha kuwa Mahakama zinaendelea kukabiliwa na ongezeko la
mashauri, ambayo mengi kati yake yanaweza kutatuliwa kwa haraka, kwa gharama
nafuu, na kwa maridhiano, bila kupitia mchakato mrefu wa mashauri, hivyo
kuokoa gharama na muda ambao utatumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Alieleza kuwa upatanishi wa Mahakama umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwezesha
migogoro kumalizika kwa haraka na kila mmoja ni mashuhuda wa ongozeko la migogoro
inayomalizika katika hatua ya upatanishi ambayo kwa sasa inazidi asilimia 50, tofauti na
hali ilivyokuwa miaka minne nyuma.
‘Hali hii inatupa matumaini na chachu ya kuendelea kuwajengea uwezo Mahakimu na Wadau wa
usuluhishi ili kuongeza ufanisi katika kutatua migororo kupitia upatanishi na kufikia
malengo yaliyopo katika dira ya 2050 ya kutumia njia hii katika kuleta amani na
utulivi katika jamii zetu pamoja na kuchangia katika uchumi endelevu,’ alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza
pia kuwa upatanishi unaofanyika nje na ndani ya Mahakama
hauondoi mamlaka ya Mahakama, bali unaikamilisha na kusaidia upatikanaji wa haki, kuondoa mrundikano
wa mashauri, kuokoa muda na rasilimali, kulinda mahusiano ya kijamii na
kibiashara, na kuwapa wahusika nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kupata
suluhu ya migogoro.
Alisema kuwa mafunzo hayo, siyo ya kiutaratibu pekee, bali ni uwekezaji katika kujenga uwezo, maadili,
na taaluma ya wapatanishi wa Mahakama na wadau wa usuluhishi.
Mhe. Maruma alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa chuo cha IJA kwa kubali ombi lao la
kushirikiana nao katika kuendesha mafunzo hayo ambayo ni muendelezo wa juhudi za Mahakama
katika kuwajengea uwezo wa watumishi wake ili kutekeleza majukumu yao kwa
ufanisi.
‘Natambua kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mafunzo ya
upatanishi tayari yameshafanyika kwa Majaji na Mahakimu zaidi ya mia moja na
baadhi yao ndio wamekuwa wakufunzi wa mafunzo haya ambayo ni endelevu,’ alisema.
Jaji Mfawidhi alitumia
fursa hiyo pia kuwashukuru Wadau muhimu
kwa kushirikiana na Kituo katika kuwezesha mafunzo hayo bila kusita pale walipowafikia.
Alieleza kuwa hatua hiyo
inaashiria mwanzo wa ushirikiano ambao utakuwa endelevu
na kutaleta faida kubwa katika kukuza, kuongeza ufanisi na kuhamasisha si tu matumizi
ya usuluhishi katika kutatua migogoro bali hata katika kuibua changamoto zinazokwamisha
na kuzifanyia kazi kwa pamoja.
Awali, Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando, alieleza kuwa
ushiriki wa Majaji, Mahakimu, Naibu Wasajili na Wadau wa Taasisi nyingine
unaonesha kuwa usuluhishi si jukumu la mtu mmoja, bali ni juhudi ya pamoja
zinazohusika na utoaji haki.
‘Majaji na Mahakimu,
ingawa si wasuluhishi katika mashauri yao, ni wasimamizi na walezi wa mchakato
wa usuluhishi, na hivyo ni muhimu kuwa na uelewa wa kina wa misingi, taratibu
na falsafa ya mediation.
Aidha, Mhe. Mmbando
alielezea kutambua kwa heshima uwepo wa Mratibu wa Mafunzo kutoka IJA, ambaye
mchango wake ni muhimu katika kujenga uwezo wa Mahakama kupitia mafunzo
endelevu na ya vitendo.
Alieleza pia kuwa
uwepo wa TIRA katika mafunzo hayo una umuhimu wa pekee kwani bima ni miongoni
mwa sekta zinazozalisha migogoro mingi ya kibiashara na kimkataba, ambayo kwa
asili yake inafaa kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
‘Ushirikiano kati ya Mahakama na taasisi za udhibiti kama TIRA ni nguzo muhimu katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa haraka, haki, na kwa namna inayohifadhi mahusiano na kuimarisha imani ya wadau katika mfumo wa haki,’ alisema.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni