Alhamisi, 5 Februari 2026

MAHAKAMA KUU MWANZA YAADHIMISHA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI

Na. Rehema Awet – Mahakama, Mwanza

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Nimilwa Kilekamajenga amesema kuwa, Siku ya Sheria ni fursa muhimu ya kutathmini na kutafakari upya dhamira ya Mahakama katika kulinda haki za wananchi na kusimamia utawala wa sheria nchini. Aliongeza kuwa Mahakama ina nafasi ya kipekee katika kujenga jamii yenye haki, amani na maendeleo endelevu.

Aidha, alibainisha maeneo makuu ya mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya taifa kuwa ni pamoja na ulinzi wa haki za binadamu na kuimarisha utawala wa sheria, kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji, pamoja na kudumisha amani na utulivu wa kijamii.

Mhe. Kilekamajenga, alibainisha kuwa, maeneo mengine kuwa ni kuimarisha Demokrasia, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Pia alieleza kuwa maboresho ya miundombinu na matumizi ya TEHAMA katika usikilizwaji na uendeshaji wa mashauri, jambo ambalo limeongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa haki.

Kwa upande wake, Bw. Kabyemela S. Lushagara akizungumza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema Mahakama ni Mhimili muhimu wa Dola unaochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia ulinzi wa haki, utawala wa sheria na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Alioneza kuwa, Mahakama huru, yenye weledi na uadilifu huongeza imani ya wananchi na wawekezaji, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, mwakilishi huyo kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema, mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya haki, ikiwemo kupungua kwa msongamano wa mashauri, ongezeko la Majaji na Mahakimu, matumizi ya mifumo ya TEHAMA kama e-filing, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na Taasisi za utoaji haki. Pia alisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mfumo imara wa utoaji haki unaofanya kazi kwa ufanisi na kwa wakati

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Mwanza, Wakili Erick Mutta alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa uhuru wa Mahakama na ulinzi wa Mawakili wa Kujitegemea kama nguzo ya Utawala wa Sheria. Wakili Mutta alieleza kuwa Mahakama inayofanya kazi kwa haki na bila upendeleo hujenga imani ya wananchi na kuleta utulivu wa kijamii na kisiasa unaohitajika kwa maendeleo endelevu.

Chama cha Mawakili wa Kujitegemea kanda ya Mwanza ilitumia jukwaa hilo kueleza mchango wake katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo, elimu ya kisheria kwa umma, pamoja na ushiriki wake katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala nje ya Mahakama.

Mgeni rasmi ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza Mhe. Kilekamajenga alihitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wote wa haki kushirikiana kwa karibu na Mahakama ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati kwa usawa na kwa mujibu wa sheria, kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika mkoani Mwanza kwa yakibeba kauli mbiu isemayo “Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.” yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyombo vya Dola, wataalamu wa sheria pamoja na wananchi.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akiwa tayari kwa ukaguzi wa Gwaride maalum kuashiria uzinduzi wa mwaka mpya wa shughuli za kimahakama kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026. Waliosimama nyuma ni Majaji, Mawakili na sehemu ya Wadau wengine wa Mahakama Kanda ya Mwanza.

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Dkt Ntemi Kilekamajenga wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kanda ya Mwanza.

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Dkt Ntemi Kilekamajenga wakiwa katika picha ya pamoja na mawakili wa serikali na wa kujitegemea.

Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Dkt. Ntemi Kilekamajenga (katikati), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda (wa tatu kushoto) na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akihutubia wananchi katika  viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kanda ya Mwanza  kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Ntanda akihutubia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza kwenye  maadhimisho ya siku ya sheria nchini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt  Ntemi Kilekamajenga akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama, 2026.

Mgeni Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Dkt. Ntemi Kilekamajenga wakiwa anapokea heshima kutoka kwa kiongozi wa gwaride maalum la heshima siku ya maadhimisho ya siku ya sheria nchini. 

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni