Jumatatu, 23 Machi 2026

JAJI MFAWIDHI GEITA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAHAKAMA ZA WILAYA

Na DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, amefanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama za Wilaya za Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale, kwa lengo la kujionea hali halisi ya uendeshaji wa mashauri pamoja na nidhamu ya Watumishi.

Katika ziara hiyo, Jaji Mhina aliwapongeza Watumishi wa Mahakama hizo kwa kutekeleza maelekezo ya kuhakikisha kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa mwaka 2026 inaongezeka.

Aliwasisitiza kuwa wahakikishe wanavuka mwaka 2026 bila kuwa na mashauri kwa Mahakama za Mwanzo kama walivyofanya mwaka 2025 kwa kumaliza mwaka wakiwa wamemaliza mashauri yote yaliyokuwa yamefunguliwa. Aidha, alisifu hatua ya kutokuwepo kwa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili katika usikilizaji wa mashauri.

Pamoja na pongezi hizo, Jaji Mhina alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa viwanja pamoja na nyumba za Mahakama zisizotumika ili kuzuia uvamizi na upotevu wa mali za Taasisi. Aliwahimiza Viongozi na Watumishi kutafuta matumizi mbadala ya viwanja vilivyo wazi ili kuongeza tija na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Vilevile, aliwataka Viongozi wa Mahakama kuendelea kujadili masuala ya maadili katika vikao vya ndani ili kuimarisha utendaji kazi na kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa mashauri.

Katika ziara hiyo, Jaji Mhina aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Fredrick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila, pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Cleofas Waane na Maofisa wengine.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila, aliwataka watumishi kuendelea kuzingatia taratibu za ununuzi wa Serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi (NeST) ili kuhakikisha uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma.

Jaji Mhina na wajumbe wake walitembelea pia mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Masumbwe kwa lengo la kukagua maendeleo yake.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Jaji Mhina alisema kuwa jengo hilo linatarajiwa kuanza kutumika kabla ya Juni 2026. Alibainisha kuwa kwa sasa Mahakama ya Mwanzo Masumbwe inafanya kazi katika mazingira finyu yasiyokidhi mahitaji, hali inayowaweka Watumishi katika mazingira magumu na hatarishi kiafya na kiutendaji.

Kwa sasa, ujenzi wa jengo hilo umefikia hatua ya mwisho ya umaliziaji, ukiwa katika hatua ya upakaji rangi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Masumbwe.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Masumbwe, Mhe. Mashaka Msonogone, akitoa taarifa ya usikilizaji wa mashauri na ikama ya Watumishi Mahakama ya Mwanzo Masumbwe.

Mtendaji wa Mahakama Geita akisisitiza Watumishi kufuata taratibu za ununuzi kupitia Mfumo nunuzi (NeST) ili kuongeza uwazi na ufasi kwa rasilimali za umma.

Hakamu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bukombe, Mhe. Zawald Nyekelela, akitoa taarifa ya mashauri Mahakama ya Wilaya ya Bukombe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Kevin Mhina, akijadiliana na Mtendaji wa Mahakama Geita, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbogwe namna ya kuweka uzio kwenye jengo la Mahakama ya Mwanzo Masumbwe.

    Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni