Jumanne, 24 Machi 2026

JAJI NKWABI APONGEZA WATUMISHI KWA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA VIONGOZI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi amewapongeza watumishi wa Mahakama za Wilaya Kanda ya Kigoma kwa kuzingatia majukumu yao na kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa ngazi mbalimbali za Mahakama hususani ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Mhe. Nkwabi aliyasema hayo hivi karibuni katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya na Magereza, huku akisisitiza kuwa, maelekezo ya Viongozi yanapaswa kuzingatiwa kwakuwa ndio mwelekeo wa kasi ya shughuli za Mahakama ili kuhakikisha usikilizwaji wa mashauri unafikiwa kwa viwango vya juu. 

Ameongeza kuwa, maelekezo yanayotolewa na Viongozi ndio kichocheo cha utendaji wa Mahakama na hivyo kuwa katika nafasi ya juu katika usikilizwaji na umalizwaji wa mashauri Mahakamani kwa mwaka 2025-2026.

Aidha, ametoa rai kwa Viongozi wa Mahakama hizo kusimamia vema mashauri ya mirathi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha za mirathi haziendelei kuonekana katika akaunti ya Mahakama badala yake walipwe wanufaika na Mahakama ihakikishe msimamizi anawajibika kuisaidia Mahakama kufunga mirathi mara baada ya kugawa mirathi kwa wanufaika wa mirathi husika.

Alisema kwamba, hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa fedha na malalamiko mahakamani lakini pia amewataka watendaji kufuatilia vema malipo ya mirathi kwani ndio wanaohusika na ulipwaji wa fedha za mirathi, hivyo ni vema kuwa na mawasiliano ya karibu kati ya Hakimu husika na jalada la shauri pamoja na Maafisa Masuhuli wanaoendelea kufanya malipo ya fedha za wanufaika hao kupitia nyaraka halisi za Mahakamani.

Jaji Nkwabi na Viongozi wa Kanda ya Kigoma na Wilaya Kasulu walitembelea ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Heru Juu na kukagua maeneo ya mipaka ya Mahakama hiyo ambayo ujenzi upo zaidi ya asilimia 76 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Mkizingatia taratibu zote za usimamizi wa mashauri ya mirathi hakika fedha za mirathi zaidi ya shilingi za Kitanzania 201,868,074.66 iliyopo kwenye akaunti ya mirathi ya Kigoma itaisha na haitaongezeka tena na suala hilo litabaki historia kwa Kanda ya Kigoma, hivyo nashauri Maafisa wapitie jalada kwa jalada ili kubaini wanufaika hatimaye fedha hiyo ilipwe mapema kwa wadau hao,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kigoma   Bw. Filbert Matotay wote katika nyakati tofauti walisisitiza umuhimu wa kuzingatia ufungaji wa mirathi kwa mujibu wa taratibu pamoja na kufuatilia kwa karibu wasimamizi wa mashauri hayo ili kuondoa sintofahamu katika hatua ya ufungaji wa Mirathi.

Vilevile, waliweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha zoezi hilo la ufungaji wa mirathi linafanyika kwa ufanisi na ndani ya muda waliojipangia ndani ya Kanda ili kuendana na muda wa maelekezo ya Viongozi wa juu wa Mahakama.

Mahakama zilizokaguliwa kwanzia tarehe 16 hadi 20 mwezi 03, 2026 ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mahakama ya Wilaya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe, Kakonko na Gereza la Kilimo Kwitanga.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma , Mhe. John  Nkwabi akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kakonko alipoanzia ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva  Mushi akitoa ufafanuzi wa moja ya mambo aliyokuwa akiulizwa na
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, alipokuwa akikaguliwa hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akifanya utambulisho wa watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (hayupo katika picha) wakati wa ukaguzi wa Mahakama hiyo.

Ukaguzi ukiendelea.....

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ni Maofisa Waandamizi wa Magereza (wa pili na wa tatu kutoka kulia na wa tatu kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,  Mhe. Fadhili Mbelwa (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Kigoma, Bw. Filbert Matotay mara baaada ya ukaguzi wa Gereza la Kilimo Kwitanga.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,  Mhe. Fadhili Mbelwa (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Kigoma, Bw. Filbert Matotay  (wa pili kulia)Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mhe. Ambikile Kyamba (wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kakonko (wa kwanza kulia) na waliosimama ni sehemu ya watumishi wa Mahakama hiyo mara baaada ya ukaguzi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama hiyo ya Wilaya Kasulu (waliosimama) mara baada ya ukaguzi. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Fadhili Mbelwa, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Kigoma, Bw. Filbert Matotay, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi, na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya  Kasulu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya-Uvinza. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Kigoma, Bw. Filbert Matotay, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Misana Majula  na wa kwanza kulia ni Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Bw. Tumaini Panga.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni