Na FRANCISCA SWAI - Mahakama Musoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, amewaasa Watumishi kufanya
kazi kwa weledi, kuzingatia na kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Viongozi
wa ngazi mbalimbali za Mahakama.
Mhe. Mtulya alitoa wito
huo hivi karibuni katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama ndani ya Kanda ya Musoma,
huku akisisitiza maelekezo ya Viongozi yanapaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha
utoaji wa haki unafikiwa kama inavyokusudiwa.
Aidha, aliwapongeza Watumishi
kwa mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa ndani ya Kanda kutokana na kuzingatia
maelekezo ya Viongozi yliyosababisha kutokuwa na Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo
kwenye Magereza yote.
Alisema kuwa jambo hilo limesaidia
kupunguza msongamano gerezani, lakini pia kuwaruhusu Washtakiwa ambao
wangelazimika kukaa Mahabusu kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, huku
wakiendelea pia na mashauri yao mahakamani.
Pamoja na pongezi hizo,
Mhe. Mtulya na Viongozi alioambatana nao katika ukaguzi huo, ambao ni Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora na Mtendaji wa Mahakama
Kuu Musoma, Bw. Leonard Maufi, walisisitiza umuhimu wa kuzingatia ufungaji wa
mirathi kwa mujibu wa taratibu.
Viongozi hao waliwekeana
mikakati mbalimbali ya kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi na ndani
ya muda waliojiwekea.
Vilevile, Mhe. Mtulya
aliwapongeza Watumishi kwa namna wanavyojitoa kushiriki matukio mbalimbali ya
kijamii pamoja na safari za utalii wa ndani zinazopangwa ndani ya Kanda.
‘Pamoja na kuwa tunatumia
muda wetu mwingi kazini, ni muhimu kushiriki matukio hayo ili kujenga umoja na
mshikamano, kutunza kumbukumbu nzuri za pamoja, kuongeza ari, tija na mahusiano
bora kati ya Watumishi,’ alisema.
Katika ukaguzi huo, Mhe.
Mtulya alitembelea ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Serengeti pamoja na
kukagua maeneo na mipaka ya Mahakama mbalimbali ndani ya Kanda ya Musoma.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) akisikiliza kwa makini maelezo yanayotolewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Leonard Maufi (aliyesimama) wakati wa kikao na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Butiama.Muonekano wa jengo linalojengwa la Mahakama ya Wilaya Serengeti.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni