Jumatatu, 30 Machi 2026

JAJI NDUNGURU AIKABIDHI KANDA YA NJOMBE KWA JAJI VICTORIA NONGWA

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru amekabidhi ofisi ya Mahakama Kuu Kanda mpya ya Njombe kwa Jaji Victoria Mlonganile Nongwa ambaye ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi.

Makabidhiano ya Masjala ndogo ya Mahakama Kuu Njombe  ambayo itaanza kutoa huduma zake rasmi kuanzia tarehe 30 Machi, 2026 yalifanyika Ijumaa tarehe 27 Machi, 2026 mbele ya watumishi wote  w Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Wilaya nne (4) ambazo ni Ludewa, Wanging’ombe, Makete pamoja na Makambako.                                                                                                     

Aidha akiwa katika kikao cha makabidhiano, Mhe. Ndunguru  alimpongeza Mhe. Jaji Nongwa kwa kuteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe huku akishukuru kwa kupunguziwa majukumu ya mashauri ya rufaa ambazo zilikuwa zikitokea Njombe kwenda Mahakama Kuu Iringa.

Pamoja na hayo alizungumza na watumishi wote wa Mahakama za Mkoa wa Njombe kupitia mfumo wa mkutano mtandao (Video Conference) kwa ambao hawakuweza kufika katika kikao hicho cha makabidhiano hayo.

Kadhalika, Jaji Ndunguru alitoa pongezi kwa watumishi wote hususani kwa ushirikiano mkubwa  waliompa kwa kipindi chote alichokuwa akihudumu kwa Mahakama zote za Mkoa wa Njombe na Wilaya zake na kuwaomba ushirikiano waliompa yeye kwa kipindi chote wampe pia na Jaji Nongwa ambaye ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Victoria Mlonganile Nongwa alimpongeza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa pamoja na kuwashukuru watumishi wote wa Mahakama za Mkoa wa Njombe kwa kumpa ushirikiano Jaji Ndunguru ambaye amehudumu kwa kipindi chote ambacho amekuwa akisimamia Mahakama za Mkoa wa Njombe ambaye kwa sasa atahudumu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa pekee.

 Aidha, Mhe. Nongwa aliwasisitiza na kuwaomba watumishi wote wa Mahakama mkoani Njombe kumpa ushirikiano pamoja na kusisitiza watumishi watumie mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuachana na matumizi ya peni na karatasi katika utendaji kazi pamoja na kuwahudumia wananchi vizuri hasa makundi maalum mfano walemavu na akina mama wajawazito.

Tukio la makabidhiano ya Kituo cha Mahakama Kuu Njombe lilihudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Bw. Richard Mbambe, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama pamoja na Afisa Bajeti wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Wilaya zake, Bw. Juma Nyenzi.

Aidha, Viongozi hao walitoa neno la shukrani kwa pamoja wakati wa makabidhiano hayo mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa.

Awali Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe pamoja na Wilaya zake zote zilikuwa chini ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa. Mahakama inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za uboreshaji huduma ikiwemo ujenzi wa majengo ya Mahakama ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania  kanda ya Iringa,  Mhe. Dunstan Ndunguru (kushoto) akikabidhi kitabu cha makabidhiano ya Mahakama Kuu Masjala ndogo mpya ya Iringa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe Mhe. Victoria Mlonganile Nongwa.

 Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda ya Iringa,  Mhe. Dunstan Ndunguru akisaini kitabu cha wageni wakati  alipofika Mahakama ya  Hakimu Mkazi Njombe kabla ya makabidhiano  ya Kituo cha Masjala ndogo ya Mahakama Kuu Njombe.

 Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda mpya ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akisaini kitabu cha wageni  alipofika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.

Kutoka  kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano, katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa na  anayefuata upande wa kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku wakiwa kwenye kikao cha makabidhiano ya Mahakama Kuu Kanda mpya ya Njombe.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda mpya ya Njombe,  Bw. Richard Mbambe akisoma taarifa pamoja na ratiba ya kikao hicho pamoja na  kuwakaribisha Majaji Wafawidhi mkoani Njombe.

 Watumishi wa Mahakama ya  Hakimu Mkazi  Njombe pamoja na Wilaya zake wakifuatilia kilichokuwa kinajiri kwenye kikao cha pamoja cha  makabidhiano ya Kituo cha Mahakama Kuu Kanda ya Njombe.

Meza Kuu ikiongozwa na 
Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu pamoja na watumishi wa kada mbalimbali baada ya kumalizika kikao cha makabidhiano ya Kituo cha Mahakama Kuu Kanda ya Njombe. Wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe,  Mhe. Victoria Nongwa, wa tatu kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku, wa pili kulia ni  Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Mhe. Joseph Luambano, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Bw. Richard Mbambe.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni