Jumapili, 29 Machi 2026

JAJI PROJESTUS KAHYOZA AWAAGA WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA

  •  Awashukuru watumishi wote Kigoma
  • Awasisitiza kufanya kazi kwa maadili bila kuacha nyuma mazoezi kwa afya

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza tarehe 24 Machi, 2026 aliwaaga watumishi wa Kanda hiyo mara baada ya kupata uhamisho wa Kituo cha kazi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kuelekea Kanda ya Tabora.

“Nimepokea barua ya uhamisho wa kituo cha kazi ikinihamisha kutoka Kigoma kuelekea Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, hivyo naomba kuwaaga na kutoa shukrani kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Augustine Rwizile na Mhe. John Nkwabi na watumishi wote kwa ushirikiano wenu wa dhati katika kipindi chote nilichohudumu katika Kituo hiki cha Kigoma,” alisema Jaji Kahyoza.

Vilevile, alitoa rai kwa watumishi wote wa Mahakama Kanda ya Kigoma kutoaacha kufanya mazoezi ya viungo kwani ndio mtaji na msingi wa ufanisi na tija katika shughuli za mfanyakazi kwa mwajiri wake.

Aidha, alisema kuwa, ataendelea kuwa mdau wa mazoezi na huko aendako kwani afya ndio jambo muhimu la kwanza kwa mwanadamu, hivyo ameisisitiza Klabu ya Mazoezi Kigoma iendelee kwakuwa ndio msingi wa utendaji kazi wenye tija kwa mwajiri.

kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Kanda ya Kigoma, alimshukuru na kumtakia kila la heri Jaji Kahyoza katika kituo chake kipya.

Alimshukuru pia kwa ushirikiano wake kwa kipindi chote alipokuwa akihuduma katika kituo cha Kigoma na hivyo kumtaka kuendelea na juhudi zake za kupiga kazi kama alivyofanya Mahakama Kanda ya Kigoma.

“Kuondoka kwa Mhe. Kahyoza kunapunguza nguvu katika usikilizwaji wa mashauri katika Kanda yetu, hata hivyo Kanda tumejipanga kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa yanasikilizwa na kuamriwa kwa haraka ili kuendana na Dira ya Mahakama ya Utoaji wa Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo,” alisema Jaji Rwizile.


Jaji Projestus Kahyoza akizungumza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma juu ya uhamisho wake na kutoka Kanda hiyo na kuhamishiwa Makahama Kanda ya Tabora.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakipokea taarifa ya uhamisho wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

Jaji Kahyoza (wa kwanza kulia) akiwaaga wanamazoezi  katika eneo la kufanyia mazoezi lililopo juu ya jengo la Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) na  Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga  wakipiga zoezi la (push up) wakati wakimuaga mwanamazoezi mwenzao, Mhe. Kahyoza. Waliosimama ni watumishi wanamazoezi wa Kanda hiyo wakati wa kuwaaga wanamazoezi wenzao  Mhe. Projestus Kahyoza, na aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama, Bw. Filbert Matotay (aliyevaa fulana la kahawia) ambaye naye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Singida.

Picha ya wanamazoezi wakifurahia kinywaji maalum kwa ajili ya kuwaaga wanamazoezi wenzao wanaohamishwa Kituo cha kazi ambao ni  Jaji, Mhe. Projestus Kahyoza na  Bw. Filbert Matotay, Mtendaji wa Mahakama.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni