Na Mwandishi wetu, New York-Marekani
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) hivi karibuni kilielezea ni kwa vipi kinachagiza matumizi ya teknolojia kwa
lengo la kuhakikisha haki mahakamani kwa jamii hususan kwa wanawake na
wasichana inapatikana kwa wakati.
Wakizungumza wakati wa kikao cha kando kwenye Mkutano wa 70
wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 jijini New York, Marekani,
chama hicho kilisema kinafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mageuzi ya
Mahakama nchini Tanzania.
Kikao hicho cha kando kilikuwa na maudhui Kutatua
vikwazo vya kijinsia kwenye haki kupitia mahakama ya mtandao nchini
Tanzania, ambapo walitaja mageuzi hayo kuwa ni pamoja na mifumo ya
kidijitali na mahakama za mtandaoni.
Muda wa kusikiliza kesi umepungua
“Kupitia uwekezaji katika teknolojia na ubunifu wa mifumo ya
TEHAMA, Mahakama nchini Tanzania zinaendelea kuwa jumuishi zaidi, zenye
ufanisi, na rafiki kwa watumiaji—hasa wanawake na manusura wa ukatili wa
kijinsia, (GBV),” amesema Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Barke Sehel
ambaye pia ni Mwenyekiti wa TAWJA iliyoanzishwa mwaka 2000 na kusajiliwa rasmi
mwaka 2022
“Hatua kubwa iliyopigwa ni pamoja na uhifadhi wa kidijitali
wa zaidi ya mafaili 10,000 ya zamani jijini Dar es Salaam, jambo lililopunguza
muda wa kutafuta mafaili kutoka wiki kadhaa hadi dakika chache. Maboresho haya
yameongeza kasi ya upatikanaji wa haki na kupunguza ucheleweshaji wa kesi
unaowaathiri zaidi wanawake na makundi yaliyo hatarini,” alisema Mwenyekiti
huyo wa TAWJA.
Kiini cha mabadiliko ni nini?
Kiini cha mabadiliko haya ni Mfumo wa Kielektroniki wa
Usimamizi wa Mashauri (JoT e-CMS), unaorahisisha shughuli zote za mahakama kwa
njia ya kidijitali.
“Mfumo huu unaruhusu ufungaji wa mashauri kwa njia ya
mtandao (e-filing), ufuatiliaji wa kesi kwa wakati halisi, na
upatikanaji wa kumbukumbu za kesi kwa urahisi.” Alieleza Jaji Sehel.
Hali kadhalika mfumo huo umewezesha kupanga kazi kiotomatiki
ikiwa ni pamoja kugawa mashauri kwa MajajI, kupanga ratiba za usikilizwaji na
utoaji wa taarifa kwa wahusika. “Faida zake ni pamoja na upatikanaji
wa huduma saa 24, kupunguza gharama za uendeshaji, na kupunguza makosa ya
kibinadamu katika usimamizi wa kesi,” alifafanua Mwenyekiti huyo
wa TAWJA.
Faida za mahakama mtandao
Wakati wa kikao hicho iliwekwa bayana ni kwa kiasi gani
TEHAMA inaboresha haki pamoja na matumizi ya akili unde (AI) katika kurekodi,
kutafsiri na kushughulikia ushahidi.
“Hii imepunguza kwa kiasi kikubwa maumivu ya
kisaikolojia kwa manusura wa GBV kwa kuepusha kurudia simulizi za matukio
yanayowapatia kiwewe,” alisema Jaji Sehel.
Faida zingine za Mahakama Mtandao ni kuruhusu mashahidi
kushiriki katika shauri wakiwa mbali, ndani na nje ya nchi. Aidha, katika Makao
Makuu ya Mahakama yaliyopo Dodoma, kuna chumba maalum cha Kanzi Data au
Data Hub kinachowezesha uchambuzi wa taarifa za shauri kwa wakati halisi,
ikiwemo mashauri ya GBV.
Jambo lingine lililozungumziwa ni mfumo wa “Sema
na Mahakama” unaotoa fursa kwa wananchi kutoa maoni au malalamiko
kupitia simu au mtandao, huku Programu ya Mahakama za Mwanzo ikitoa takwimu za
moja kwa moja kwa ajili ya ufuatiliaji na maamuzi.
Kuwezesha Wanawake Kupitia Haki za Kidijitali
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kimesisitiza
kuwa, matumizi ya teknolojia si tu kwa ajili ya kuboresha utendaji bali pia ni
nyenzo muhimu ya kuhakikisha haki za wanawake zinazingatiwa. Kupitia mifumo hiyo,
gharama zinapungua, faragha inaongezeka na mazingira ya haki yanakuwa salama zaidi kwa
wanawake.
Hata hivyo, Chama hicho kimeonya kuwa, matumizi ya
teknolojia yanapaswa kuzingatia usawa ili kuepuka kuongeza changamoto mpya kwa
makundi yaliyo pembezoni.
Teknolojia isijenge ukuta kati ya wa mijini na vijijini
Ni kwa mantiki hiyo Hakimu wa Mkoa, Zanzibar na pia Mratibu
wa TAWJA huko Zanzibar, Sara Omar Hafidh alizungumzia umuhimu wa mafunzo
endelevu kwa watendaji wa Mahakama.
“Sote tunajua kuwa kujifunza kubonyeza kitufe sahihi
kwenye kompyuta ni jambo rahisi. Lakini sehemu ngumu ni kuendesha mahakama ya
mtandaoni kwa huruma na uelewa. Tunawafundisha majaji na mahakimu wetu
kushughulikia majeraha ya kisaikolojia kupitia skrini, kuhakikisha kwamba hata
katika mazingira ya kidijitali kila mwananchi anahisi kuonekana, kusikilizwa,
na kuheshimiwa,” alisema Mratibu huyo wa TAWJA, Zanzibar.
Jambo lingine ni kuhakikisha mifumo ya kidijitali
ina ulinzi madhubuti wa taarifa.” Ni dhahiri kuwa mtu aliye katika hali ya
hatari akihisi kuwa taarifa zake binafsi zinaweza kuvuja, ataogopa kujitokeza.
Hivyo, dunia yetu ya kidijitali lazima iwe salama na isiyopenyeka. Teknolojia
inapaswa kuwa ngao ya ulinzi—ngao inayowalinda walio dhaifu, si mwanga
unaowaweka wazi,” alisema.
Mafunzo yanayotolewa na TAWJA
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) na Katibu Msaidizi wa TAWJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda
alisema Chama hicho ndicho cha kwanza kuanzisha mafunzo kwa watendaji wa
Mahakama nchini Tanzania miaka ya 2000.
“Mafunzo haya yanayotolewa kwa ushirikiano na Mahakama ya
Tanzania yanalenga pamoja na mambo mengine kujenga uwezowa majaji, mahakimu,
waendesha mashtaka,askari polisi, magereza na wachunguzi wa kesi,” alisema.
Kupitia mafunzo hayo, washiriki hupewa maarifa na ujuzi wa
vitendo unaohitajika kushughulikia kesi zenye mwelekeo wa kijinsia, ikiwemo
ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono, talaka na migogoro ya ndoa,
ukatili dhidi ya watoto na matunzo yao, pamoja na masuala ya mirathi, na
ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Washiriki pia hufundishwa jinsi ya kuepuka kuongeza maumivu
ya kisaikolojia kwa manusura wa unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia,
kwa kudhibiti mwenendo wa mahakama na kukusanya ushahidi kutoka kwa manusura
kwa njia inayolinda utu wao, ili kufikia maamuzi ya haki.
Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Katibu Msaidizi wa TAWJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza jambo kwenye kikao cha kando cha CSW70 kilichofanyika hivi karibuni jijini
New York nchini Marekani kuhusu Kutatua Vikwazo vya Kijinsia kwenye haki kupitia
Mahakama Mtandao.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni