Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, imeungana na wanawake wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya ziara ya kijamii katika Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira.
Maadhimisho hayo ambayo hufanyika tarehe 8 Machi kila mwaka yalianza kwa watumishi
wa Mahakama Kuu kushiriki pamoja na wanawake wengine katika siku hiyo muhimu
inayolenga kutambua mchango wa wanawake katika jamii.
Maadhimisho hayo yalibeba na kauli
mbiu inayosema, “Haki kwa wanawake na wasichana msingi wa maendeleo
jumuishi kufikia dirĂ¡ 2050.”
Baada ya kushiriki
katika maadhimisho hayo, watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro walifanya
ziara maalum ya kutembelea Gereza la Wanawake Kingolwira lililopo mkoani
Morogoro.
Ziara hiyo
iliongozwa na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Janeth
Kinyage, ikiwa na lengo la kuwafariji wanawake waliopo
gerezani hapo pamoja na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya
kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku wakiwa gerezani.
Watumishi hao
walipata fursa ya kujumuika na wanawake waliopo gerezani hapo, kushirikiana nao
katika mazungumzo ya faraja pamoja na kuonesha upendo na mshikamano kama sehemu
ya kuadhimisha siku hiyo ya wanawake duniani.
Ziara hiyo pia
ilikuwa na lengo la kuwapa moyo na matumaini wanawake hao kuwa bado wana nafasi
ya kujifunza, kujirekebisha na kuendelea na maisha baada ya kumaliza vifungo
vyao.
Akizungumza katika
ziara hiyo, Mratibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza ambaye pia ni Mkuu wa
Gereza la Wanawake Kingolwira, Afande Nimwindael
Mzirai, aliwashukuru watumishi wa
Mahakama kwa moyo wao wa kujali na kuwafikia wanawake waliopo gerezani.
Alisema kuwa ujio huo umeleta faraja kubwa kwa wafungwa hao na
umeonesha mshikamano wa kijamii kwa wanawake wote bila kujali hali walizonazo.
Aidha, alitoa wito
kwa watumishi wa umma pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kuheshimu sheria
za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha kuvunja
sheria na hatimaye kujikuta wakitumikia vifungo gerezani.
Aliongeza kuwa
gereza hilo pia ni sehemu ya kujifunza na kujenga upya maisha, ambapo wanawake
waliopo hapo hupatiwa mafunzo mbalimbali ya stadi za maisha kama vile kilimo,
ushonaji wa cherehani pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji ili kuwa na
ujuzi utakaowasaidia wanaporejea katika jamii.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo,
Mhe. Kinyage aliwahimiza wanawake waliopo gerezani kuwa na uvumilivu, nidhamu
pamoja na matumaini katika kipindi chote cha kifungo chao. Aliwaasa kutumia
muda wao wakiwa gerezani kujifunza mambo yatakayowasaidia kujenga maisha mapya
pindi watakapomaliza vifungo vyao.
“Msijisikie
wanyonge kwa kuwa hapa, kwani kila changamoto ina mwisho wake. Muhimu ni
kujifunza, kuwa na nidhamu na kujiandaa kwa maisha bora baada ya kutoka hapa,”
alisema Mhe.Kinyage
Maadhimisho hayo
pamoja na ziara hiyo yameonesha mshikamano, upendo na kujali kwa watumishi wa
Mahakama kwa wanawake wote katika jamii, ikiwemo wale waliopo katika mazingira
ya kifungo, huku yakilenga kuhamasisha matumaini, marekebisho na mshikamano wa
kijamii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni