Jumatatu, 9 Machi 2026

WATUMISHI WANAWAKE MAHAKAMA YA TANZANIA WAHIMIZWA KUENDELEZA UADILIFU NA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA

       Ni katika Hafla ya Usiku wa Wanawake wa Mahakama-Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

   Jaji Masabo awahimiza pia kujiendeleza kimasomo 

Na HALIMA MNETE & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Wanawake watumishi wa Mahakama ya Tanzania wamehimizwa kuendelea kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kuendeleza juhudi za kukuza usawa wa kijinsia katika Mhimili huo.

Wito huo umetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Juliana Masabo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya Watumishi wanawake wa Mahakama ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08 Machi 2026 kwenye Ukumbi wa Cathedral jijini Dodoma, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kufungua hafla hiyo, Mhe. Dkt. Masabo aliwashukuru wanawake wote waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo, huku akibainisha kuwa, ushiriki wao unaonesha dhamira ya dhati ya wanawake wa Mahakama katika kuimarisha mchango wao katika utoaji wa haki kwa jamii.

Alisema Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo yalianza kuadhimishwa mwaka 1911, yanalenga kuikumbusha jamii kuhusu nafasi, haki na mchango wa mwanamke katika maendeleo ya jamii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jaji Masabo, kuna jumla ya watumishi wanawake 342 katika Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani, Masjala Kuu, Divisheni za Mahakama Kuu pamoja na Mahakama Kuu Dodoma (IJC) wanaofanya kazi katika nafasi mbalimbali ikiwemo Majaji, Naibu Wasajili, Wakurugenzi, Mahakimu, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji, Wakuu wa Vitengo pamoja na kada nyingine za utumishi.

Aidha, ilielezwa kuwa, katika Mhimili wa Mahakama kuna maendeleo yanayoonekana katika usawa wa kijinsia kwenye nafasi za uongozi ambapo takwimu zinaonesha, kwamba kati ya Majaji 39 wa Mahakama ya Rufani, Wanawake ni 13 sawa na asilimia 33, huku katika Majaji 104 wa Mahakama Kuu wanawake wakiwa 40 sawa na asilimia 38.

Kadhalika, kati ya Naibu Wasajili 82 waliopo wanawake ni 42 sawa na asilimia 51, jambo linaloonesha ongezeko la ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ndani ya Mhimili huo.

Katika hafla hiyo, Watumishi wanawake wa Mahakama walipongezwa pia kwa kushiriki matendo ya huruma kwa kutembelea watoto wenye mahitaji maalum katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, ambapo walitoa msaada wa mahitaji mbalimbali pamoja na kugharamia matibabu ya mtoto mchanga aliyekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Akizungumzia, Maadhimisho ya mwaka huu, Mhe. Dkt. Masabo alisema Kaulimbiu ya mwaka 2026 inayosema, “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050” inapaswa kuwa chachu kwa wanawake kujitathmini namna wanavyotekeleza wajibu wao katika kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa katika utoaji wa huduma za haki.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza wanawake kuendelea kupendana, kusaidiana na kuinuana ili kuwa daraja la mafanikio kwa wanawake wengine, huku akitoa wito kwa Menejimenti ya Mahakama kuendelea kuwaamini na kuwapa fursa zaidi za uongozi na maendeleo ya kitaaluma.

Aidha, kupitia maadhimisho hayo washiriki walipata fursa ya kupata ushauri kutoka kwa Mkufunzi katika Masuala ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa-Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka kuhusu umuhimu wa usawazishaji wa majukumu ya kazi na familia (work-life balance), elimu inayolenga kuwasaidia wanawake kuboresha afya ya akili, kuimarisha utendaji kazi kazini pamoja na kuendeleza ustawi wa familia.

Watumishi wanawake walioshiriki katika sherehe hiyo ni kutoka Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani, Masjala Kuu, Divisheni za Mahakama Kuu pamoja na Mahakama Kuu Dodoma (IJC).

Matukio katika picha Hafla ya Usiku wa Wanawake wa Mahakama-Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Juliana Masabo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wanawake wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma katika hafla ya Usiku wa Wanawake wa Mahakama katika kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Irene Msokwa na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mwajabu Mvungi.

Sehemu ya Watumishi wanawake wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika hafla ya Usiku wa Wanawake wa Mahakama kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani jana tarehe 08 Machi, 2026 kwenye Ukumbi wa Cathedral uliopo jijini Dodoma.

Burudani ikiendelea...
Wanawake wakionesha vipaji vyao katika Siku yao muhimu.

Muda wa Dua ukawadia.

 Kamati ya Maandalizi katika ubora wake.


Ukataji keki maalum zilizoandaliwa kwa ajili ya kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2026.

Masuala ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa-Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka akitoa mada kwa watumishi wanawake wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika Usiku wa Wanawake wa Mahakama-Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni