Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita
Timu ya mpira wa
miguu ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita imeibuka na ushindi wa mabao 3–2 dhidi ya
Timu ya Mawakili kutoka Mwanza katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Machi 7,
2026.
Mchezo huo
ulifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi na Sekondari St. Aloysius
vilivyopo Shilabela, Manispaa ya Geita, ambapo timu hizo zilionyesha ushindani
mkubwa na burudani kwa mashabiki waliohudhuria.
Katika mchezo huo,
bao la kwanza la Mahakama Kuu Geita lilifungwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa
Mahakama ya Wilaya ya Nyang’hwale, Robert Nyando. Bao la pili lilifungwa na
Ateba Stephano huku bao la tatu likifungwa na Mhasibu wa Mahakama Kuu Geita, Goodluck
Machange.
Kwa upande wa Timu
ya Mawakili Mwanza, bao la kwanza lilifungwa kwa njia ya penalti na Wakili Fredrick
Magaiwa baada ya mlinda mlango wa Mahakama Kuu Geita kushika mpira ndani ya
eneo la hatari. Bao la pili lilifungwa na Wakili Hensen Emmanuel.
Akizungumza baada
ya mchezo huo, Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Geita, Griffin
Mwakapeje, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita,
aliwakaribisha wageni hao katika Mahakama Kuu Geita na kuwashukuru kwa
kushiriki mchezo huo.
Alisema lengo la
michezo hiyo ni kuimarisha mahusiano, ushirikiano na kubadilishana mawazo kati
ya Wadau wa sekta ya sheria.
“Nia ya mashindano
haya ni kutuleta pamoja, tusahau kwa muda majukumu ya kesi na kujumuika katika
kujenga ushirikiano pamoja na kubadilishana mawazo. Pia inaonyesha kuwa licha
ya majukumu mengi ya kisheria tuliyonayo, bado tunashiriki kikamilifu katika michezo,”
alisema Jaji Mwakapeje.
Aidha, alimshukuru
Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Geita, Fredrick Lukuna, kwa
kuratibu na kufanikisha mashindano hayo. Aliongeza kuwa baada ya ujio wa
Mawakili wa Mwanza mjini Geita, watumishi wa Mahakama Kuu Geita pia watafanya
ziara ya kwenda Mwanza kwa ajili ya michezo kama sehemu ya kuimarisha
ushirikiano huo.
Aliwasihi
Mawakili wa Mwanza kuangalia uwezekano wa kusaidia Mkoa wa Geita kupata chapter
yake ya Chama cha Mawakili ili kuimarisha shughuli za kisheria na ushirikiano
katika ukanda huo.
Kwa upande wake,
Rais wa Chama cha Mawakili (Mwanza Chapter) aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu
Geita kwa kukubali mwaliko na kushiriki mchezo huo.
Alisema licha ya
timu yao kupoteza, wamefurahishwa na kiwango cha wachezaji wao na wameuchukulia
mchezo huo kama fursa ya kuimarisha timu yao pamoja na afya za Mawakili.
Aliongeza kuwa
hatua za Mkoa wa Geita kuwa na chapter yake ya Chama cha Mawakili
zinaendelea vizuri, huku akiwakaribisha watumishi wa Mahakama Kuu Geita
kutembelea Mwanza kwa ajili ya mchezo mwingine wa kirafiki siku zijazo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni