Jumatatu, 9 Machi 2026

WAFANYAKAZI WANAWAKE WA MAHAKAMA YA TANZANIA WAWAGUSA WATOTO NJITI BENJAMIN MKAPA

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, watumishi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma tarehe 06 Machi, 2026 walitembelea watoto njiti (premature) wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Watoto hao ni wale waliozaliwa kabla ya wakati na waliokuwa wakipatiwa huduma hospitalini hapo wakiwa na umri wa kuanzia siku moja hadi siku 28 tangu kuzaliwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi wa Mahakama, Bi. Gladness Godwin Massawe alisema lengo la wanawake kutembelea Hospitali hiyo ni kujionea hali ya watoto hao pamoja na kutambua umuhimu wao katika jamii.

Alisema katika kuadhimisha siku hiyo waliamua kushiriki katika tendo la kijamii kwa kuwatembelea watoto hao na kuwapatia baadhi ya mahitaji muhimu pamoja na kugharamia matibabu ya mtoto mmoja aliyekuwa akipatiwa huduma katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU).

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya kuonesha upendo, mshikamano na kuwapa matumaini watoto hao pamoja na familia zao.

Wakati huohuo akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dkt. Rehema Yona alishukuru kwa msaada huo.

"Msaada huu umeleta faraja na matumaini kwa watoto pamoja na wazazi wao na umeonesha moyo wa upendo na kujali jamii," alisema Dkt. Rehema huku akiwatakia heri na baraka kwa kuendelea kushirikiana na jamii katika kusaidia wenye uhitaji.

 Watumishi wanawake wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma tarehe 06 Machi, 2026. 

Watumishi wanawake wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakielekea wodini kuona watoto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).

 

    Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Gladness Massawe akizungumza jambo mara baada ya kupokelewa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.


    Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi wa Mahakama, Bi Gladness Massawe (wa pili kushoto) akikabidhi zawadi kwa  Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Rehema Yona mara baada ya kuwasili katika hospitali hiyo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Rehema Yona akitoa shukrani mara baada ya kupokea wageni hao.





Sehemu ya watumishi wanawake kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika zoezi la utoaji msaada kwa watoto njiti waliopo Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 08 Machi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni