Ijumaa, 13 Machi 2026

MSAJILI MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA ASISITIZA UMUHIMU WA KUTUMIA TEKNOLOJIA MAHAKAMANI

Na JAMES BUSANYA & HALIMA MNETE- Mahakama Dodoma.

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama.

Mhe. Herbert ametoa msisitizo huo leo tarehe 13 Machi, 2026, wakati anafunga mafunzo ya siku tano kati ya Maofisa wa Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar yaliyokuwa yanafanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma.

Msajili wa Mahakama ya Rufani ameeleza kuwa teknolojia inaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa kazi pamoja na kupunguza muda wa usikilizaji wa mashauri.

“Ni muhimu kuendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika Mahakama zetu, ikiwemo usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mfumo wa kielektroniki, jambo ambalo linaweza kusaidia kuondoa mlundikano wa mashauri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki,” amesema.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mhe. Herbert amewasihi washiriki kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha utendaji kazi ndani ya Taasisi zao na kuimarisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Amesema kuwa mafunzo ya kubadilishana uzoefu ni muhimu katika kujenga uwezo wa watumishi wa Mahakama, hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji pamoja na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Naye Naibu Mrajisi wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Faraji Shumari Juma, akizungumuza kwenye hafla hiyo alitoa shukrani kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu, akisema kuwa yamewasaidia washiriki kupata maarifa na uzoefu mpya wa kiutendaji.

Aidha, aliomba ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar uendelee kuimarishwa ili kusaidia Taasisi hizo kujifunza zaidi kutoka kwa kila upande.

Alieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu hasa katika kuboresha matumizi ya mifumo ya kiteknolojia kwenye uendeshaji na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Wakati wa mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza tangu tarehe 9 Machi, 2026, washiriki wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya utendaji kazi, matumizi ya mifumo ya kidijitali, maadili ya kazi pamoja na mbinu za kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama.

Washiriki wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kutumia maarifa hayo katika kuboresha utendaji wa kazi katika Mahakama zao.

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert, akizungumza wakati anafunga mafunzo hayo leo tarehe 13 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma.

Naibu Mrajisi wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Faraji Shumari Juma, akitoa neno la shukrani kwenye hafla hiyo.

Sehemu ya Washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mahkama ya Zanzibar wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim (katikati). Wengine ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert (kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kinabo Minja.


Sehemu ya Washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini) ikiwa kwenye picha ya pamoja. Aliyekaa ni Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni